Tony Pulis afichua siri ya Wenger

Muktasari:

Pulis, ambaye ana uhusiano mzuri na Wenger na aliishuhudia timu yake ikiichapa Arsenal mabao 3-1, ametoboa siri ambayo mashabiki wa Arsenal hawatapenda kuisikia kwa sasa kuhusu kocha wao ambaye wanataka aondoke.

DUNIANI hakuna siri ya watu wawili, na kama ipo basi usimwambie siri yako mtu anayeitwa, Tony Pulis, kocha wa klabu ya West Brom ambaye Jumamosi aliibuka na ushindi wa nyumbani katika pambano dhidi ya Arsenal.

Pulis, ambaye ana uhusiano mzuri na Wenger na aliishuhudia timu yake ikiichapa Arsenal mabao 3-1, ametoboa siri ambayo mashabiki wa Arsenal hawatapenda kuisikia kwa sasa kuhusu kocha wao ambaye wanataka aondoke.

Pulis amedai alizungumza na Wenger wakati wa pambano hilo na kocha huyo Mfaransa amemwambia kwamba, atasaini mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha Arsenal msimu ujao.

“Nitashangaa kama ataondoka,” alisema Pulis mara baada ya mechi hiyo akizungumzia hatma ya Wenger. Alipoulizwa ni kwanini anasema hivyo, alijibu: “Kwa sababu aliniambia hivyo. Nadhani ni kocha bora zaidi, ambaye Arsenal wamewahi kuwa naye. Ndiyo wanaweza kumaliza ndani ya timu nne za juu na kutwaa Kombe la FA, unadhani hivyo ni vibaya?

“Sidhani kama heshima ni jambo la maana siku hizi. Watu wanaishi kwa ajili ya leo. Kama utaniuliza Arsenal wafanye nini basi mimi sio mtu sahihi wa kumuuliza.”

Katika pambano hilo, mashabiki wanaompinga Wenger walipitisha ujumbe wa kutaka kocha huyo asipewe mkataba mpya. Ujumbe huo ulipitishwa katika anga la Uwanja wa Harthowns kwa ndege ndogo wakati pambano likiendelea.

Mara baada ya mechi hiyo, Wenger aliwaambia waandishi wa habari kuwa, tayari ameshaamua kuhusu hatma yake ya baadaye na ataitangaza muda mchache ujao kwa mashabiki wenye hasira na yeye klabuni hapo.

Wakati huo huo, imebainika kuwa uhusiano wa Wenger na kiungo mchezeshaji Mesut Ozil, umedorora baada ya staa huyo kuiambia klabu hiyo kwamba, ana mpango wa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani.

Ozil alikuwa katika kambi ya Arsenal Ijumaa asubuhi, lakini akajiondoa na kwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai kwamba, misuli yake ilikuwa inamuuma.

Matokeo yake aliachwa katika kikosi cha kwanza kilichoanza mechi hiyo na nafasi yake ilichukuliwa na kiungo wa kimataifa wa Wales, Aaron Ramsey.

Wakati Arsenal ikiamini kwamba, Ozil asingeweza kujiunga na kambi ya Ujerumani, staa huyo alikuwa amepanga kujiunga na kambi ya timu yake ya taifa jijini Dortmund kwa maandalizi ya pambano dhidi ya England, Jumatano.

Wenger pia yuko matatizoni na staa wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez, ambapo inasemekana uhusiano wao umefika pabaya kama ilivyo kwa Ozil, anaweza kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Wenger alijiunga na Arsenal mwaka 1996 na tangu hapo amekuwa mmoja kati ya makocha wenye mafanikio makubwa kwenye Ligi Kuu England.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, heshima yake imeanza kuyeyuka klabuni hapo baada ya Arsenal kutochukua ubingwa wa England kwa kipindi cha miaka 13.

Mkataba wake unatazamiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na endapo atasaini mpya, kuna uwezekano tukio hilo likapokewa kwa chuki kubwa na mashabiki wa Arsenal, ambao wanaonekana wamemchoka kutokana na matokeo mabovu ya kikosi chake.