TUHUMA : Mwamuzi wa Clasico naye utata

Muktasari:

  • Sasa kuna zengwe limeibuka kuhusu mwamuzi wa pambano la mahasimu wa jadi wa Hispania Real Madrid na Barcelona.
  • Wanakutana keshokutwa katika Uwanja wa Nou Camp huku Madriod wakiwa na pointi sita mkononi mbele ya Barcelona.

MAJUZI tu kulikuwa na zengwe la mwamuzi katika pambano la Liverpool na Manchester United pale Anfield.

Sasa kuna zengwe limeibuka kuhusu mwamuzi wa pambano la mahasimu wa jadi wa Hispania Real Madrid na Barcelona.

Wanakutana keshokutwa katika Uwanja wa Nou Camp huku Madriod wakiwa na pointi sita mkononi mbele ya Barcelona.

Hata hivyo, vyombo vya habari vya Hispania vimetoa macho kwa uteuzi wa mwamuzi, Carlos Clos Gomez kuchezesha pambano hilo kwa madai kwamba, amekuwa akiipendelea sana Barcelona.

Barcelona haijawahi kupoteza pambano lolote ambalo mwamuzi huyo amechezesha huku ikiwa imeshinda mechi 17 na kutoa sare tatu katika mechi 20 ambazo amewahi kuwachezesha.

Gomez pia amewazawadia Barcelona penalti nne huku akitoa mbili dhidi yao. Hakuna mchezaji wa Barca aliyewahi kumpa kadi nyekundu.

Kwa upande wa Madrid hali sio nzuri sana anapochezesha Gomez.

Amewachezesha mechi 27 na wamefungwa mechi nne huku wakishinda mechi 18.

Hajawahi kuwaonyesha kadi nyekundu na amewapa penalti tano huku akiwa hajatoa penalti hata moja dhidi yao.

Kocha wa zamani wa Madrid, Jose Mourinho, ambaye kwa sasa yupo Manchester United akiendelea kupambana na waamuzi, Desemba 2010 alidai kwamba mwamuzi huyo alifanya makosa 13 dhidi yao wakati timu hiyo ikiichapa Sevilla 1-0 huku wachezaji tisa wa Madrid wakipewa kadi za njano.

Hata hivyo, licha ya uvumi huo kuwa anawapendelea Barcelona, kocha wa Madrid, Zinedine Zidane ameshusha pumzi kwa mashabiki wa timu yake akidai kwamba haamini kuwa mwamuzi anaweza kupendelea timu na akataka akili ipelekwe mchezoni zaidi.

“Siamini katika madai haya kuwa mwamuzi yeyote anaweza kuipendelea klabu moja au nyingine. Nadhani itakuwa mechi nzuri huku mwamuzi akifanya kazi yake vyema. Sifuatilii shutuma hizo za upendeleo na sina wasiwasi. Nataka niifikirie mechi tu,” alisema Zidane.

“Watu wanataka kuiona mechi nzuri Jumamosi huku mwamuzi akifanya kazi yake vizuri,” aliongeza kocha huyo ambaye timu yake imecheza mechi 31 katika michuano mbalimbali bila ya kufungwa mpaka sasa.

Katika pambano hilo, Zidane atamkosa winga wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale ambaye alifanyiwa operesheni ya kifundo cha mguu Jumanne nchini England baada ya kuumia katika pambano la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Sporting Lisbon na anatazamiwa kukaa nje kwa wiki nne hadi sita.

Wakati Madrid wakiwa na habari hiyo mbaya, Barcelona wamepata habari nzuri baada ya kocha wao, Luis Enrique kuweka wazi kwamba kiungo wao mkongwe, Andres Iniesta atarudi uwanjani baada ya kuumia goti mwezi uliopita na alirudi mazoezini Ijumaa.

“Andres anasubiri apewe ruhusa na madaktari, lakini ni suala la kukamilisha taratibu tu. yupo fiti na amefanya mazoezi na sisi. Atapatikana kwa ajili ya uteuzi wa wachezaji watakaocheza,” alisema kocha huyo.