Steven Gerarrd astaafu soka

Muktasari:

Gerrard, nahodha wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England, ameamua kutundika daluga zake juu baada ya miaka miwili ya kucheza katika Ligi Kuu ya Marekani na klabu ya LA Galaxy ambapo mkataba wake ulikoma wiki mbili zilizopita.

IMETOSHA. Ndiyo kauli pekee unayoweza kuitumia kurahisisha sentensi nyingi alizotumia mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote katika soka la England na Ulaya, Steven Gerrard alipotangaza kustaafu kucheza soka la kulipwa jana.

Gerrard, nahodha wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England, ameamua kutundika daluga zake juu baada ya miaka miwili ya kucheza katika Ligi Kuu ya Marekani na klabu ya LA Galaxy ambapo mkataba wake ulikoma wiki mbili zilizopita.

Gerrard mwenye umri wa miaka 36, aliyezaliwa kitongoji cha Whiston jijini Liverpool mnamo Mei 30, 1980 alicheza soka la kiwango cha juu sana pale Anfield kwa muda wa miaka 17 huku akifanikiwa kuibuka mmoja kati ya viungo wa nguvu zaidi kuwahi kutokea klabuni hapo, Ligi Kuu England na duniani kwa jumla.

“Kutokana na uvumi mwingi ambao umekuwa ukizunguka katika vyombo vya habari kuhusu hali yangu ya baadaye, naweza kuthibitisha kwamba nimestaafu kucheza soka la kulipwa. Nilikuwa na maisha mazuri ya soka na nashukuru kwa kila kipindi nilichopitia Liverpool, timu ya taifa ya England na LA Galaxy.

“Nikiwa mdogo nilitimiza ndoto zangu za kukipiga katika jezi maarufu nyekundu ya Liverpool, na nilipocheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya Blackburn Rovers Novemba 1998 sikutazamia kama ningeweza kucheza kwa miaka 18,” alisema Gerrard.

Akiwa na Liverpool, Gerrard aliichezea klabu hiyo ya Merseyside mechi 710 akifunga mabao 186. Alikuwa nahodha wa kikosi cha Liverpool kilichofanya maajabu katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya AC Milan kwa kurudisha mabao yote matatu angali wakiwa wamefungwa mabao 3-0 hadi mapumziko.

Baadaye Liverpool ilitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa matatu na kuishangaza dunia hasa kwa wale mashabiki ambao, waliachana na luninga zao na kwenda kulala wakiamini kuwa pambano hilo lilikuwa limemalizika wakati wa mapumziko.

Achilia mbali taji hilo kubwa la maisha yake ya soka, Gerrard pia alitwaa mataji mawili ya kombe la FA, matatu ya kombe la Ligi, moja la Uefa na pia taji la Uefa Super Cup.

Alicheza mechi 114 katika kikosi cha England akiwa nahodha katika kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini 2010 na kile kilichoshiriki Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Bahati mbaya kwa Gerrard ni kwamba hakuweza kupata mafanikio yoyote na vikosi hivyo kama ilivyo kwa wachezaji wengine mahiri wa kizazi chake nchini humo.

Mechi yake ya kwanza katika kikosi cha England alicheza mwaka 1998 na kutokana na uhodari aliouonyesha alifanikiwa kutajwa katika kikosi cha England kilichoshiriki michuano ya Euro 2000 iliyofanyika katika nchi za Ubelgiji na Uholanzi ambapo, Ufaransa iliibuka kuwa bingwa wa michuano hiyo.

Alichukua unahodha Liverpool mwaka 2003 akichukua nafasi ya nahodha wa zamani, Sami Hyypia ambaye alikuwa mlinzi wa kimataifa wa Finland na tangu hapo Gerrard aliiongoza Liverpool kwa zaidi ya miaka 10.

Anaondoka katika soka akiwa mmoja kati ya wachezaji mahiri wachache katika Ligi Kuu England ambao, hawakuwahi kutwaa taji hilo. Fursa pekee ya kulikaribia kutwaa taji hilo ilikuwa ni katika msimu wa 2013-14 wakati Liverpool ilipofukuzana na Manchester City mpaka katika dakika za majeruhi.

Bahati mbaya katika pambano dhidi ya Chelsea April 27, 2014 Gerrard aliteleza katika eneo la hatari la timu yake na kumruhusu mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal, Demba Ba kufunga kwa urahisi bao la kuongoza la Chelsea kabla ya Willian kufunga bao la pili na kuua matumaini ya Liverpool kutwaa ubingwa huo.