SIO MIMI: Vardy akanusha kuwa mchawi wa Ranieri

Muktasari:

  • MIEZI tisa tu iliyopita kulikuwa na raha kubwa pale Leicester, lakini sasa kimenuka. Ni mwendo wa kumtafuta mchawi tu baada ya kufukuzwa kwa kocha aliyeipa ubingwa, Claudio Ranieri siku tatu zilizopita

MIEZI tisa tu iliyopita kulikuwa na raha kubwa pale Leicester, lakini sasa kimenuka. Ni mwendo wa kumtafuta mchawi tu baada ya kufukuzwa kwa kocha aliyeipa ubingwa, Claudio Ranieri siku tatu zilizopita.

Inasemekana baadhi ya wachezaji wa Leicester City walikuwa na kauli kubwa iliyotoa shinikizo kwa mmiliki wa Leicester City, Vichai Srivaddhanaprabha pamoja na mwanaye ambaye ni Makamu Mwenyekiti, Aiyawatt Srivaddhanaprabha kumfukuza kazi Muitaliano huyo.

Mmoja kati ya wachezaji wanaotajwa kuwa nyuma ya kufukuzwa kwa Ranieri ni mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Jamie Vardy ambaye msimu uliopita alifunga mabao 24 yaliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuipa ubingwa Leicester.

Mwingine ni kipa wa timu hiyo, Kasper Schmeichel. Lakini hata hivyo, Vardy amejitokeza hadharani kukanusha vikali madai hayo kuwa alihusika kwa kiasi kikubwa kumfukuzisha kazi Ranieri ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Leicester.

“Uvumi kwamba nilihusika na kufukuzwa kwake ni uongo mkubwa, sio ukweli na unaumiza sana. Nimeandika na kufuta maneno mengi sana kabla ya kutuma ujumbe huu. Nahitaji maneno mazuri zaidi ya kumuandika vema Claudio,” aliandika Vardy.

“Claudio daima nitampatia heshima zangu zote. Tulichofanikiwa pamoja kama timu ilionekana kama vile hakiwezekani. Aliniamini wakati watu wengi hawakuniamini na kwa hilo nampa shukrani za ndani za moyo wangu. Kitu pekee ambacho kinatupa hatia kama timu ni kwamba tumeshindwa kufanya vizuri msimu huu na hilo tunakubali hadharani na katika vyumba vya kubadilishia nguo. Tutafanya kila tuwezalo kurekebisha. Namtakia Claudio mafanikio mema siku za usoni. Asante Claudio kwa kila kitu,” alimaliza Vardy.

Maelezo hayo yamekuja licha ya habari kutoka katika vyumba vya kubadilishia nguo kwamba Ranieri alijiharibia kutokana na kubadilisha mbinu zake za soka kiasi cha kuipeleka timu katika anga za kushuka daraja.

Inadaiwa kwamba kocha huyo wa zamani wa Chelsea alifahamishwa habari za kufukuzwa kwake na Mkurugenzi wa Ufundi wa Leicester City, Jon Rudkin mara tu timu hiyo iliposhuka katika Uwanja wa Ndege England ikitokea Sevilla ambako ilichapwa mabao 2-1 na Sevilla katika pambano la kwanza la mtoano la Ligi ya Mabingwa.

Katika pambano hilo, Vardy alifunga bao moja ambalo bado linaweka hai matumaini ya Leicester kusonga mbele katika pambano la marudiano wiki mbili zijazo, lakini tayari maamuzi yalikuwa yamechukuliwa na wamiliki wa timu hiyo kumfukuza Ranieri. Inadaiwa kuwa maamuzi ya kumfukuza Ranieri katika kibarua chake yalishachukuliwa na bodi ya timu hiyo tangu Februari 12 mwaka huu baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Swansea City ugenini jijini Cardiff. Juzi Ranieri alikwenda kuwaaga wachezaji wa timu hiyo pamoja na wafanyakazi wengine huku majina ya makocha wanaoweza kuchukua nafasi yake yakianza kuvumishwa katika vyombo mbalimbali vya habari.  Roberto Mancini na Gus Hiddink wanapewa nafasi ya kuchukua nafasi yake huku pia jina la kocha wa zamani wa Leicester, Nigel Pearson likipewa nafasi kwa madai kwamba kuna wachezaji wanataka arudi baada ya kutimuliwa na nafasi yake kupelekwa kwa Ranieri misimu miwili iliyopita.

Leo usiku Leicester inaingia uwanjani kwa mara ya kwanza bila ya Ranieri ndani ya misimu hii miwili na itakuwa kibarua kigumu nyumbani kwa kukipiga na Liverpool.