SHOW TIME: Moto huu nani anauzima?

KATOA NUKSI: Pogba aliifungia Man United bao la nne likiwa ni bao lake la kwanza tangu aliposajiliwa kwa rekodi ya dunia

Muktasari:

  • Paul Pogba, Phillip Coutinho na Mesut Ozil walipagawisha ile kinomanoma.

LONDON, ENGLAND

UNAHITAJI wikiendi nyingine zaidi ya iliyoisha? Ilikuwa wikiendi tamu kwa wababe wakubwa England, lakini zaidi kwa mchezaji mmoja mmoja hasa wale wa nafasi za kiungo ambao, walionyesha utamu wa soka.

Paul Pogba, Phillip Coutinho na Mesut Ozil walipagawisha ile kinomanoma.

Jumamosi Manchester United iliichapa Leicester City mabao 4-1 katika Uwanja wa Old Trafford huku wakienda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Chris Smalling, Juan Mata, Marcus Rashford na Pogba.

Hata hivyo, kivutio kikubwa katika pambano hilo alikuwa ni Pogba ambaye amenunuliwa kwa dau la Pauni 89 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto lililofungwa Septemba Mosi akivunja rekodi ya uhamisho wa dunia.

Pogba alifunga bao lake la kwanza na kucheza soka maridadi akitawanya mipira vyema na mwisho wa mechi alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa pambano hilo huku akiwaacha midomo wazi wachambuzi wa soka, Gary Neville na Graeme Souness.

“Pogba alikuwa nguzo sana katika kipindi cha kwanza. Wengi huwa tunamtazama zaidi Wayne Rooney siku hizi, lakini watu wanasema kwa dau la Pauni 90 milioni kwa mchezaji wa kiungo lazima uwe unaamua mechi. Ndicho alichofanya leo (Juzi).

“Kipindi cha kwanza alikuwa mchezaji bora uwanjani na alionekana kupania sana, kama alivyoambiwa na Mourinho arudi nyuma haraka kupora mipira. Nadhani aliamshwa wiki hii,” alisema Gary Neville.

Wakati Neville akiwa amepagawa hivyo, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alikuwa amepagawa na kiwango cha kiungo wake, Phillip Coutinho ambaye kwa mara nyingine tena alikuwa chachu ya ushindi mnono wa Liverpool wa mabao 5-1 dhidi ya Hull City katika dimba la nyumbani Anfield.

Coutinho alifunga bao moja la mita 25 huku akiunganisha vyema eneo la kiungo la Liverpool ambayo inaonekana kuwa tishio msimu huu chini ya Kocha Klopp na inapewa nafasi kubwa ya kuleta upinzani katika nafasi ya ubingwa.

“Siku zote anafunga mabao kama haya. Ningependa kupewa sifa kwa uwezo wake wa kupiga mashuti, lakini mimi sihusiki katika hilo. Mabao yote ambayo anafunga yanatokana na nafasi ambazo tunatengeneza. Katika hili alikuwa amemalizia vizuri sana. Bonge la bao,” alisema Klopp.

Wakati Pogba na Coutinho waking’ara kabla jua halijazama, kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil alikuwa staa wa pambano la usiku dhidi ya Chelsea ambapo Arsenal iliibuka kutoka katika rekodi mbovu dhidi ya Chelsea na kuichapa mabao 3-0 hadi kufikia mapumziko.

Ozil alifunga bao moja lakini alipewa alama nyingi za mchezo na mitandao mingi barani Ulaya kwa kucheza soka maridadi akiiunganisha Arsenal na kufanya manjonjo mengi uwanjani ambayo yaliwafanya viungo wa Chelsea kuwa hoi.

Pembeni mwa uwanja, Ozil alipiga chenga za maudhi kwa viungo wa Chelsea huku pia akipiga pasi ndani ya uwanja angali akitazama mashabiki jukwaani na hivyo kuwapa wakati mgumu viungo wa Chelsea hasa N’Golo Kante, ambaye makali yake yamepungua tangu atue Chelsea.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ambaye Septemba hii ametimiza miaka 20 kamili tangu alipoanza kuifundisha Arsenal mwaka 1996, alipagawishwa na kiwango cha Ozil na wenzake huku akidai hicho kilikuwa moja kati ya viwango bora chini ya utawala wake.

“Katika kipindi cha pili ilikuwa nusu nusu lakini katika kipindi cha kwanza tulionyesha kiwango bora sana. Tulicheza kwa staili, kasi na hiyo ndiyo aina ya soka tunalotaka kucheza. Ni moja kati ya viwango bora katika miaka ya karibuni,” alisema Wenger.