SHOO YA KIBABE: Mourinho na Conte kuvaana usiku kitemi

Monday March 13 2017

JOSE MOURINHO
Atamkosa mpachika mabao wake

JOSE MOURINHO Atamkosa mpachika mabao wake Zlatan Ibrahimovic anayetumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, akianza na mechi ya leo. 

 LONDON, ENGLAND. LEO usiku mida fulani hivi kuna shoo ya kibabe pale Stamford Bridge. Jose Mourinho anarudi tena na kikosi cha Manchester United kuvaana na Chelsea ikiwa ni mara yake ya pili kurudi uwanja wake huo wa zamani.

Mara ya kwanza katika pambano la Ligi Kuu England raundi ya kwanza Mourinho alipewa ubatizo wa moto. Safari hii haijulikani kitakachotokea katika pambano hili la robo fainali michuano ya FA lakini Mo ur inho atakwenda na hasira za kutosha.

Tatizo kubwa kwa United litaanzia kwa kumkosa mshambuliaji wake mbabe anayeziweza vyema shoo kama hizi, Zlatan Ibrahimovic ambaye leo ataanza rasmi adhabu yake ya kukosa mechi tatu kwa kumpiga kiwiko beki wa Bournemouth, Tyrone Mings katika pambano la Ligi Kuu wikiendi iliyopita.

Alhamisi usiku, Zlatan aliiaga United kwa wiki hizi mbili zijazo baada ya kupika bao moja katika pambano la michuano ya Europa dhidi ya Rostov na litakuwa pengo kubwa kwa Mourinho kumkosa mshambuliaji huyo ambaye anaongoza kwa kufunga mabao katika kikosi cha United msimu huu.

Wakati Mourinho akimkosa Zlatan, Kocha wa Chelsea, Antonio Conte atakuwa na kikosi chake kamili ambacho kwa sasa kinaongoza Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi 10.

Mtihani pekee kwa Conte utakuwa kama ni kuendelea kumpanga beki wake mkongwe, John Terry, nahodha wa timu hiyo ambaye tayari ameshapangwa katika mechi tatu zilizopita za FA ambazo kwa Conte zilionekana kutokuwa ngumu.

Katika pambano hili nafasi ya Terry haionekana kuwa wazi na Conte anaweza kupanga mziki wake ukizingatia kuwa mechi yake ijayo ya Ligi Kuu itakuwa siku tano zijazo dhidi ya Stoke City na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza hata wakipangwa leo watakuwa na muda wa kupumzika kwa ajili ya mechi ijayo.

 Kwa mujibu wa rekodi, Manchester United imeshinda mechi saba kati ya tisa za FA dhidi ya timu hiyo, lakini imepoteza mbili za mwisho dhidi ya Chelsea ambazo ni pambano la fainali 2007 pamoja na pambano la raundi ya sita mwaka 2013.

Kwa upande wa rekodi binafsi za Mourinho, kocha huyu Mreno ameshinda mechi nne kati ya sita dhidi ya timu ambazo aliwahi kuzifundisha awali. Moja kati ya mechi alizofungwa dhidi ya timu yake ya zamani ni ile ya raundi ya kwanza dhidi ya Chelsea ambapo alichapwa mabao 4-0 Stamford Brdige.

Katika miaka ya karibuni Chelsea imeonekana kuwa mbabe zaidi kwa Manchester United ambapo katika mechi 11 zilizopita imefanikiwa kuichapa United mara sita na kutoka sare tano. Mechi ya mwisho kupigwa na United ilikuwa Oktoba 2012 wakati ilipochapwa 3-2.

Kuonyesha kwamba hali imekuwa siyo nzuri kwa United hata kuliona lango la Chelsea imekuwa shida kidogo katika miaka ya karibuni ambapo imefunga mabao matatu tu katika mechi tisa zilizopita.

Katika mechi hizo haijawahi kufunga bao zaidi ya moja.

Pambano la leo litachezeshwa na Michael Oliver ambaye ndiye mwamuzi mdogo katika Ligi Kuu England akiwa na umri wa miaka 32 tu.

Pia aliweka rekodi ya kuwa mwamuzi mdogo zaidi kuchezesha Ligi Kuu England wakati alipochezesha pambano la Fulham dhidi ya Portsmouth mwaka 2010. Alikuwa na miaka 25 tu.

Oliver pia alikuwa mwamuzi katika pambano la Ngao ya Hisani mwaka 2014 kati ya Arsenal na Manchester City ambapo Arsenal waliokuwa mabingwa watetezi wa FA, walishinda mabao 3-0.