SAMAHANI: Babu Wenger kajishitukia kwa kituko chake aisee

Muktasari:

Wenger alimsukuma Taylor katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Burnley ambalo Arsenal ililazimika kusubiri mpaka dakika ya mwisho kabisa kufunga bao la utata la penalti katika pambano ambalo lilikuwa na matukio ya kushangaza mwisho wa mechi.

BABU amejishtukia kwamba ameharibu. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amelazimika kuwa mpole na kuomba samahani kwa jamii baada ya kujishtukia kwamba, aliharibu juzi wakati alipomsukuma mwamuzi wa akiba, Anthony Taylor.

Wenger alimsukuma Taylor katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Burnley ambalo Arsenal ililazimika kusubiri mpaka dakika ya mwisho kabisa kufunga bao la utata la penalti katika pambano ambalo lilikuwa na matukio ya kushangaza mwisho wa mechi.

Wenger alikasirishwa na penalti ambayo ilikuwa imetolewa na mwamuzi wa pambano hilo, Anthony Taylor ambaye aliamua kumpeleka jukwaani lakini kocha huyo akang’ang’ania kutazama mpira akiwa katika sehemu ya kuondokea wachezaji.

Alipofuatwa na Taylor kuambiwa apande juu jukwaani, kocha huyo Mfaransa alimsukuma Taylor. Hata hivyo, mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo alijishtukia na kuomba msamaha ingawa inaeleweka kwamba FA bado itamchukulia hatua.

“Najutia kila kitu na naomba msamaha kwa hilo. Nilitolewa kupelekwa jukwaani lakini nikadhani ningeweza kutazama mechi nikiwa katika korido. Nilitolewa kwa kitu ambacho mnakisikia kila siku katika soka,” alisema Wenger.

“Hakikuwa kitu kibaya na mara tisa kati ya kumi ukisema nilichosema huwa haupelekwi jukwaani. Nilikuwa mtulivu katika mechi yote mpaka katika dakika za mwisho. Ilinipasa nikae kimya tu kisha niingie ndani halafu niende nyumbani.” Hata hivyo, licha ya kuomba msamaha inadaiwa kuwa kwa mujibu wa kanuni Taylor hakupaswa kuendelea kumuondoa Wenger katika eneo alilopo na badala yake walinzi wa uwanjani hapo ndio waliopaswa kumwondoa kocha huyo.

Waamuzi wote hao wawili, Moss na Taylor wana rekodi ya kuwapeleka majukwaani makocha pindi wanapolalamikia sana maamuzi yao. Moss ndiye mwamuzi ambaye alimpeleka jukwaani Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho baada ya kupiga chupa ya maji kwa hasira katika pambano kati ya Manchester United dhidi ya West Ham lililomalizika kwa sare ya 1-1 Old Trafford.

Kwa upande wa Taylor, yeye katika siku za karibuni ndiye aliyempeleka jukwaani Kocha wa Stoke City, Mark Hughes katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Tottenham ambapo, timu ya Hughes ilichapwa mabao 4-0.

Hata hivyo, licha ya kasheshe hiyo, Wenger atakuwa anachekea mbavuni baada ya timu yake kushika nafasi ya pili kwa kukusanya pointi zote tatu muhimu katika dakika za majeruhi baada ya timu yake pia kupewa penalti ya utata na Mossi kufuatia faulo aliyofanyiwa mlinzi wake, Laurent Koscielny.

Penalti hiyo ilifungwa vyema na mshambuliaji wao wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez huku Arsenal ikicheza pungufu kufuatia kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kiungo wao wa kimataifa wa Uswisi, Granix Xhaka ambaye msimu huu amepewa kadi mbili nyekundu.

Kwa sasa Arsenal inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 47 huku ikiwa imeachwa nyuma na viongozi wa Ligi hiyo, Chelsea ambao wana pointi 55 baada ya kushinda katika pambano la baadaye dhidi ya Hull City lililopigwa katika dimba la Stamford Bridge.

Katika pambano hilo mabao mawili ya mshambuliaji mtata, Diego Costa aliyerudishwa kikosini na kocha, Antonio Conte baada ya kukwaruzana naye hivi karibuni, pamoja na jingine lililofungwa na mlinzi, Gary Cahill yalitosha kuizamisha Hull ambayo ilileta upinzani mkubwa katika pambano hilo ambapo ilicheza soka la nguvu ikipambana kuondoka mkiani.

Katika pambano lijalo Arsenal itaendelea kuwa nyumbani kwa kukipiga na Watford wakati Chelsea nayo itakuwa nyumbani kukipiga na Liverpool katika pambano linalotazamiwa kuwa kali pamoja na kutoa picha halisi ya ubingwa msimu huu.