Ruud Gullit adai Leicester City wamejitakia wenyewe

Muktasari:

Ruud Gullit, staa wa zamani wa Chelsea ambaye pia amewahi kuwa kocha mchezaji wa Chelsea, amedai kwamba kosa walilofanya Leicester msimu huu ndio kosa ambalo kocha aliyepita wa Chelsea, Jose Mourinho alilifanya msimu uliopita.

UNAIONEA huruma Leicester City? Inawezekana uko sahihi, lakini mtu mmoja mwenye roho mbaya amesema ‘shauri zao’ na wanastahili kukipata walichokipata kwa sababu hawakujifunza somo ambalo Chelsea ilipitia mwaka jana.

Ruud Gullit, staa wa zamani wa Chelsea ambaye pia amewahi kuwa kocha mchezaji wa Chelsea, amedai kwamba kosa walilofanya Leicester msimu huu ndio kosa ambalo kocha aliyepita wa Chelsea, Jose Mourinho alilifanya msimu uliopita.

Gullit anaamini kuwa Leicester ilihitaji changamoto mpya ikiwemo kuwauza mastaa wake na kuibadili timu, lakini ikang’ang’ania kukaa na mastaa wale wale baada ya kutwaa ubingwa wa England na baadhi kati yao wameridhika na mishahara mikubwa.

“Ilikuwa ni hadithi ya kusisimua lakini walijua kwamba wasingerudia tena mwaka unaofuata. Vardy alikuwa anawindwa na Arsenal, Kante alifanya uamuzi sahihi kuondoka, Mahrez alitaka kuondoka lakini akaamua kubaki,” alisema Gullit.

“Bingwa, hata kama akiwa timu kama Chelsea, unashinda ubingwa na mwaka unaofuata mambo yanakuwa mabaya. Unahitaji kununua sura mpya, unahitaji wachezaji wapya. Kama haufanyi hivyo unajiingiza katika hali hiyo. Kuna wachezaji walikuwa wanalipwa Pauni 30 milioni lakini sasa wanapata Pauni 100,000 kwa wiki”

“Habari hapa ni kwamba kama hawawezi kurudia basi wangewauza tu. Tazama kilichotokea Chelsea. Kitu kilekile tu. Walishinda ubingwa na msimu uliofuata wakachemsha. Unahitaji kukichangamsha. Klabu nzuri zinanunua wachezaji wazuri kwa ajili ya kupeleka ujumbe kwa wachezaji wazuri kwamba ‘Kama hautakazana tutachezesha hawa’.

Hiki ndicho kilichotokea Chelsea. Ghafla Moses anacheza, Pedro anacheza. Wachezaji ambao wangeweza kuwa benchi sasa,” alisema Gullit.

Juzi Leciester City walichapwa mabao 2-0 na Swansea City ugenini na kujikuta wakiangukia nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu England huku wakiwa na pointi moja tu zaidi dhidi ya Hull City ambao wanashika nafasi ya 18.

Kichapo cha Leicester City juzi kinawafanya wawe mabingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kupoteza mechi tano mfululizo tangu Chelsea ilipofanya hivyo Machi 1956. Leicester pia wamecheza mechi 15 za ugenini bila ya kushinda.

Leicester pia ndio timu pekee katika madaraja manne ya soka England kutofunga bao lolote tangu kuingia kwa mwaka 2017. Kinachoumiza zaidi ni kwamba muda kama huu msimu uliopita walikuwa wametoka kuichapa Manchester City na kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano lakini katika pambano dhidi ya Swansea wachezaji tisa walioanza mechi dhidi ya Manchester City walianza dhidi ya Swansea.

Kocha wa Leicester, Claudio Ranieri amekiri kwamba huenda akaanza kuwasugulisha benchi mastaa wa kikosi chake ambao walitamba msimu uliopita kwa vile ameshawapa nafasi kubwa lakini hawajazitumia.

“Inawezekana, inawezekana. Ni ngumu wakati unapofikia mafanikio mazuri unataka kuwapa tena nafasi moja, mbili au tatu. Lakini sasa imezidi. Ni kweli kwamba naweza kufanya mabadiliko kwa sababu kwa jinsi ilivyo ni ngumu kuendelea,” alisema Ranieri.

“Kila wakati nikiongea na wachezaji na wachezaji wakiongea na mimi siku zote tunajiamini tunaweza kubadili hali. Lakini sasa kuna mechi chache mbele yetu za kutafuta suluhisho haraka sana. kuna mechi mbili mbele yetu, moja ni ya Kombe la FA na nyingine ya Ligi ya Mabingwa. Lakini akili yetu kwa sasa tumeielekeza katika Ligi Kuu England.”