Rooney ndiye gwiji rasmi Man United

London, ENGLAND. JOSE Mourinho amesema Wayne Rooney sasa ni gwiji la Manchester United baada ya bao lake la kusawazisha alilofunga dhidi ya Stoke City juzi uwanjani Britannia kuandika historia mpya kwenye klabu hiyo ya Old Trafford.

Rooney, aliyetokea benchi kwenye mchezo huo, bao hilo alilofunga limemfanya afikishe mabao 250 na hivyo kumpiku Sir Bobby Charlton, ambaye alikuwapo kwenye mechi hiyo ya Stoke kushuhudia rekodi yake iliyodumu kwa miaka 44 ikivunjwa.

Rooney sasa ndiye mfungaji bora wa kihistoria wa Man United na kocha Mourinho alisema: “Mtaanza kuizungumzia rekodi ya Wayne leo, kesho na kila wakati. Ni wazi ni gwiji wa klabu, gwiji kwenye historia ya soka la Uingereza.  “Rekodi tayari ameshaiweka mfukoni, sasa anapaswa awe kawaida tu na aendelee kutufungia mabao. Tunafahamu ameweka rekodi bora kabisa, kitu ambacho hakika huwezi kukisahau.” Rooney, pia alivunja rekodi ya Charlton kwenye timu ya taifa ya England kwa kufunga mabao mengi na kwamba, jana Jumapili alipaswa kupewa zawadi yake kwa kufikia mafanikio hayo na Chama cha Waandishi wa Habari.