Ronaldo anatisha aweka rekodi

Muktasari:

Hakuna mchezaji anayecheza kwa sasa, ambaye amefunga idadi hiyo ya mabao katika timu yake ya taifa na kuna wachezaji watatu tu wa zamani wa Ulaya ambao, wamefunga idadi kubwa ya mabao kuliko Ronaldo katika timu zao za taifa.

LISBON, URENO. UMPENDE usimpende, lakini siku moja utakuja kumkumbuka Cristiano Ronaldo na hata vitabu vya kumbukumbu vitakumbuka mtoto huyu wa Kireno. Juzi aliandika rekodi nyingine huku akiendelea kunyemelea ufalme fulani wa rekodi ya kimataifa.

Ronaldo alifunga mabao mawili katika pambano la kufuzu kwenda Kombe la Dunia dhidi ya Hungary juzi huku Ureno ikishinda 3-0 na kwa kufanya hivyo, alifikisha mabao 70 katika mechi 136 alizoichezea timu ya Taifa ya Ureno.

Hakuna mchezaji anayecheza kwa sasa, ambaye amefunga idadi hiyo ya mabao katika timu yake ya taifa na kuna wachezaji watatu tu wa zamani wa Ulaya ambao, wamefunga idadi kubwa ya mabao kuliko Ronaldo katika timu zao za taifa.

Wachezaji hao ni staa wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose, ambaye aliiifungia Ujerumani mabao 71, Sandor Kocsis aliyeifungia timu ya Taifa ya Hungary mabao 75, pamoja na staa mwingine wa Hungary, Ferenc Puskas ambaye alifunga mabao 84.

Ronaldo pia anaongoza kwa ufungaji mabao katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia kuelekea Russia 2018 ambapo, mpaka sasa ana mabao tisa katika mechi tano alizoichezea nchi yake ya Ureno, ikiwa ni mabao mawili zaidi kwa mtu ambaye anamfuatia.

Ronaldo pia ameendelea kukamata baadhi ya takwimu za kutisha katika timu ya Taifa ya Ureno ambayo alitwaa nayo taji la Euro, Ufaransa mwaka jana, likiwa ni taji la kwanza kubwa la Ureno katika michuano ya kimataifa.

Kuanzia mwanzo wa mwaka jana, Ronaldo ameifungia Ureno mabao 14 katika mechi 14 ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila mechi anayoichezea Ureno. Pia, ndiye mchezaji pekee katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia aliyefunga mabao kwa mguu wa kushoto, wa kulia, kichwa, penalti pamoja na kufunga akiwa nje ya boksi.

Ronaldo aliichezea Ureno mechi ya kwanza Agosti 2003 akiwa na miaka 18. Kwa sasa ndiye mchezaji aliyeichezea Ureno mechi nyingi zaidi katika historia ya timu hiyo ya taifa na juzi lilikuwa pambano lake la 136.

Ameiwakilisha Ureno katika michuano saba mikubwa ambapo, katika michuano ya Euro ameshiriki mara nne katika miaka ya 2004, 2008, 2012 na 2016 huku akishiriki Kombe la Dunia katika miaka ya 2006, 2010 na 2014.

Ronaldo ni mchezaji wa kwanza wa Ureno kufikisha mabao 50 ya kimataifa na kwa kufanya hivyo, aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ureno. Alipewa unahodha wa Ureno Julai 2008, na kuisaidia Ureno kufika nusu fainali za michuano ya Euro 2012 akiibuka kuwa mfungaji bora. Novemba 2014 alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa michuano ya Euro kwa ujumla pamoja na mechi za kufuzu akifunga mabao 23. Katika michuano ya mwaka jana iliyofanyika Ufaransa, Ronaldo alikuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za michuano hiyo. Lakini, pia katika michuano hiyo hiyo Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga fainali nne mfululizo za michuano hiyo akianzia michuano ya 2004 iliyofanyika kwao Ureno.

Ronaldo pia alifikia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika michuano hiyo akifikia rekodi ya mkali wa zamani wa Ufaransa, Michel Platini. Ronaldo ambaye alipokea taji la Euro kama nahodha alipewa pia kiatu cha fedha.