Robert lewandowski naye mtegoni

Monday January 9 2017

 

Munich,Ujerumani. KUNA ugonjwa mmoja hatari sana umezikumba klabu za Ulaya kwa sasa, unaitwa Wachina. Ni presha.

Hata klabu zile vigogo zilizozoeleka kwa kutumia pesa, jasho linawatoka. Wachina hawataki mchezo kabisa na Wanamwaga pesa kama wamechanganyikiwa na hawaogopi kabisa.

Kwa sasa, presha imekuwa kubwa kwa klabu vigogo Ulaya, kuanzia Manchester United hadi Real Madrid, kwamba pengine hadhi tu ndiyo inayowabeba hadi sasa, lakini sio pesa. Wachina wanafanya kufuru hatari!

Stori ya hivi karibuni ni kwamba, wakala wa straika matata wa Bayern Munich, Robert Lewandowski amefichua kuwa amepata ofa ngumu sana kuigomea ambayo inamfanya mteja wake kuwa mwanasoka anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani.

Wakala, Cezary Kucharski amesema fowadi, Lewandowski amepewa ofa ya kulipwa mshahara unaozidi Pauni 32 milioni kwa mwaka anaolipwa Carlos Tevez klabuni Shanghai Shenhua, ambao unamfanya awe mchezaji anayevuta pesa nyingi zaidi kwenye mshahara duniani kwa sasa.

Alisema: “Wakala anayepeleka wachezaji China alinipigia simu. Hakuniambia jina la klabu, lakini kama ‘Lewi’ atakubaki kwenda China mshahara wake utakuwa zaidi ya Pauni 35 milioni kwa mwaka, kwa maana atakuwa anamzidi mshahara Carlos Tevez.

“Ipo wazi, si tu Lewandowski ni mdogo kiumri, bali pia ni mchezaji mzuri kuliko Tevez.”

Kutokana na pesa hiyo, wakala huyo wa Lewandowski alisema hawezi kupuuzia mpango huo wa mteja wake kwenda kucheza soka China. Tevez kwa wiki anapokea Pauni 615,000, ambao ni mkubwa.

Akimzungumzia Lewandowski, wakala huyo alisema: “Kwa sasa sawa unaweza kusema hauzwi, lakini si kwamba haiwezekani daima. Maisha siku zote yanakupa mambo mengi.”

Lewandowski hivi karibuni alisaini mkataba Bayern Munich ambao unamfanya kubaki kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Bundesliga hadi mwaka 2021, lakini hilo haliwezi kuzitisha klabu za Ligi Kuu China.

Mbali na Lewandowski klabu hizo za Wachina hivi karibuni zilimtengea kiungo wa Tottenham, Dele Alli ofa ya mshahara wa Pauni 810,000 kwa wiki kama atakubali kwenda kuichezea ligi yao.Klabu hizo za Ligi Kuu China zinajiandaa pia kuwanasa nyota kadhaa wa England, akiwamo Harry Kane, Ross Barkley na Daniel Sturridge, ambao wameambiwa kama watakubali basi mishahara yao itakuwa juu kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha mshahara anachopokea Muargentina, Carlos Tevez.