Pogba aanza kulipa pesa za Man United

POGBA

Muktasari:

  • Pogba alinunuliwa kwa dau la Pauni 100 milioni akitokea Juventus hivi karibuni, lakini alishindwa kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Bournemouth kutokana na kufungiwa katika mechi za mwisho alizocheza akiwa na Juventus msimu uliopita.

BAADA ya kelele nyingi mitaani, Paul Pogba leo ataanza kulipa madeni. Atalipa deni la pesa ambazo Manchester United imelipa katika akaunti ya Juventus. Atalipa madeni ya kelele ambazo mtaani watu wanabishana kama kweli anastahili dau alilonunuliwa au hastahili.

Kuna uwezekano mkubwa Pogba akapangwa katika pambano la leo la Ligi Kuu ya England dhidi ya Southampton baada ya yeye mwenyewe kujitangaza kuwa fiti kwa ajili ya pambano hilo na itakuwa mechi yake ya kwanza baada ya kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia hivi karibuni.

Pogba alinunuliwa kwa dau la Pauni 100 milioni akitokea Juventus hivi karibuni, lakini alishindwa kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Bournemouth kutokana na kufungiwa katika mechi za mwisho alizocheza akiwa na Juventus msimu uliopita.

Kabla ya kuanza mazoezi na United alikuwa katika likizo ndefu ya matanuzi huko Marekani baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro 2016, ambapo Ufaransa ilifika fainali, lakini sasa mwenyewe amedai yupo tayari kwa pambano la leo.

 “Inabidi umuulize kocha, lakini najisikia vizuri sana na nimefanya mazoezi kwa siku 10 sasa. Nipo poa na nimezoea hali hiyo. Miaka miwili iliyopita nilikwenda Kombe la Dunia wakati nikiwa na Juve na miaka mitatu iliyopita nilikuwa Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 20. Kwahiyo nipo poa. Ni suala la mwili wako tu na nilikuwa nafanya mazoezi wakati nikiwa likizo,” alisema Pogba.

Dau la Pogba limezua kasheshe mitaani duniani kote baada ya kuwafunika mastaa wawili wa dunia waliopita, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo ambao wote walinunuliwa na Real Madrid kwa pesa chafu kwa nyakati tofauti.

Pogba ambaye ana asili ya nchi ya Guinea barani Afrika amedai kwamba hana mawazo na dau kubwa ambalo United imelipa kwa Juventus na anataka kutwaa ubingwa wa England na pia kuirudisha United katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

“Nasikia raha kucheza mpira tu, sifikirii kabisa kuhusu hilo (Ada aliyonunuliwa). Tamaa yangu ni kuwa namba moja na kuwa bora. Lengo kubwa ni kutwaa ubingwa wa ligi. Tunataka kurudi katika Ligi ya Mabingwa kwa sababu kule ndipo tunapostahili,” alisema Pogba

Hata hivyo, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kwamba Mfaransa mwenzake huyo ana sifa zote za kucheza United licha ya uhamisho wake huo wa bei mbaya. “Thamani ya mchezaji inategemea na kipaji chake, na jinsi atakavyoiongezea nguvu timu, umri wake, na jinsi ambavyo yupo katika umri ambao anaweza kuuzwa tena,” alisema Wenger akitetea uhamisho wa kiungo huyo.

“Unapomuongelea Pogba yeye anaingia katika makundi yote haya. Lakini pia tupo katika masuala ambayo hatuwezi kuyamudu. Inabidi tutafute bei ambazo zinalipwa na watu wengine. Bei imekwenda juu kwa sababu ya upatikanaji mkubwa wa pesa,” alisema.

Kama atacheza pambano la leo, hii itakuwa mechi ya kwanza kwa Pogba baada ya miaka minne tangu alipoondoka Old Trafford Julai 2012 kwa uhamisho huru kwenda Juventus kufuatia kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza chini ya Sir Alex Ferguson. Kuanzia hapo ameibuka kuwa mmoja kati ya viungo bora duniani huku akisifika kwa ukabaji mzuri na kupeleka mipira mbele na United imelazimika kumrudisha kwa dau la rekodi ya dunia akisaini mkataba wa miaka mitano.