Ozil hat-trick, Man City yafa nne

Muktasari:

Wakati supastaa huyo wa Argentina akiondoka na zawadi hiyo ya mpira, huko Emirates, vijana wa Arsene Wenger, Arsenal wameshusha kipigo kizito, wakiichapa Lidogorets Razgrad 6-0, huku kiungo fundi wa mpira kutoka Ujerumani, Mesut Ozil akipiga ‘hat-trick’ katika mchezo huo.

LIONEL Messi ameondoka na mpira wake huko Nou Camp baada ya kufunga bao tatu, zote kwa mguu wa kushoto wakati Barcelona ilipoichapa Manchester City 4-0 kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakati supastaa huyo wa Argentina akiondoka na zawadi hiyo ya mpira, huko Emirates, vijana wa Arsene Wenger, Arsenal wameshusha kipigo kizito, wakiichapa Lidogorets Razgrad 6-0, huku kiungo fundi wa mpira kutoka Ujerumani, Mesut Ozil akipiga ‘hat-trick’ katika mchezo huo.

Iliwachukua dakika 12 tu Arsenal kuandika bao la kwanza kupitia kwa Alexis Sanchez, aliyechopu mpira kabla ya Theo Walcott kupiga la pili dakika tatu kabla ya filimbi ya mapumziko. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Arsenal iliendelea kugawa dozi kwa wapinzani wao ambapo Alex Oxlade Chamberlain akapiga bao kwenye dakika 46 kabla ya Ozil kutupia mara tatu mfululizo kwenye dakika 56, 83 na 87.

Huko Nou Camp, Pep Guardiola akiwa amerejea kumenyana na timu yake ya zamani, alikumbana na ubatizo wa moto, ambapo staa aliyemfungulia njia mwenyewe ya kutamba, yani Messi, akapiga bao lake la kwanza kwenye dakika 17 kabla ya kuongeza mengine mawili kwenye kipindi cha pili kwenye dakika 61 na 69, huku mchezo huo ukishuhudia kadi mbili nyekundu kwa kila timu na penalti moja ikikoswa. Man City ilimpoteza kipa wake Claudio Bravo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia kudaka mpira nje ya eneo lake na Barca ilimpoteza beki wao wa kati, Jeremy Mathieu, aliyekuwa ameingia kutokea benchi alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya njano mbili. Supastaa wa Brazil, Neymar alikosa penalti kwenye dakika 87, lakini dakika mbili baadaye alirekebisha makosa yake kwa kufunga bao maridadi kabisa kuhitimisha ushindi wa 4-0 kwa vijana hao wanaonolewa na Luis Enrique.

Paris Saint-Germain nao walishusha kipigo kizito kwa FC Basel baada ya kuwachapa 3-0, shukrani kwa mabao ya Angel di Maria, Lucas Moura na Edinson Cavani, wakati Napoli ikiwa uwanja wake wa nyumbani ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Besiktas na Dynamo Kiev ilikung’utwa 2-0 na Benfica. Vijana wa Brendan Rodgers, Celtic walishindwa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuchapwa 2-0 na Borussia Monchengladbach, wakati Bayern Munich walishusha kipigo cha mabao 4-1 kwa PSV. Mechi hiyo iliyofanyika Allianz Arena, Bayern ilifunga kupitia kwa Thomas Muller, Joshua Kimmich, Robert Lewandowski na Arjen Robben, wakati PSV ilifunga kupitia kwa Luciano Narsingh. Atletico Madrid walishinda 1-0 ugenini kwa FC Rostov, shukrani kwa bao la Yannick Ferreira-Carrasco.

Wakati huo huo, ratiba ya Afcon 2017 imepangwa jana ambapo Ivory Coast imepangwa pamoja na Morocco kwenye Kundi C sambamba na timu za DR Congo na Togo. Kundi A la michuano hiyo litakuwa na timu za Gabon, ambao ni wenyeji na Burkina Faso, Cameroon na Guinea Bissau, wakati kwenye Kundi B kuna timu za Algeria, Senegal, Tunisia na Zimbabwe na Kundi D linaundwa na Ghana, Mali, Misri na Uganda.