Mourinho kuwakosa nyota saba

Muktasari:

Manchester United ipo katika mbio za kuwania kumaliza katika nafasi nne za juu, ikiwa na pengo la pointi nne huku miamba hiyo ya Old Trafford ikijiandaa kukivaa kikosi cha kocha Tony Pulis, West Brom.

Jose Mourinho atakuwa na wakati mgumu kupanga kikosi chake baada ya kuwakosa wachezaji saba wa kikosi cha kwanza katika mchezo wake wa nyumbani dhidi ya West Brom.

Manchester United ipo katika mbio za kuwania kumaliza katika nafasi nne za juu, ikiwa na pengo la pointi nne huku miamba hiyo ya Old Trafford ikijiandaa kukivaa kikosi cha kocha Tony Pulis, West Brom.

Herrera akiwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa wakati wa mchezo wa robo fainali dhidi ya Chelsea katika Kombe la FA, atakosa mchezo huo.

Mfungaji bora wa kikosi hicho, Zlatan Ibrahimovic pia ataukosa mchezo huo kama sehemu ya adhabu yake aliyopewa kutokana na kumpiga kiwiko mchezaji wa Bournemouth, Tyrone Mings.

Phil Jones, Chris Smalling, Marouane Fellaini na Paul Pogba wote wanatarajiwa kuukosa mchezo huo pia kutokana na maumivu tofauti.

Licha ya Wayne Rooney kudai kuwa yupo fiti na tayari kwa kucheza, kuna wasiwasi pia kuwa ana matatizo ya goti yaliyomweka nje ya uwanja kwa wiki tatu.

Wakati pia kukiwa na mambo ya nje ya uwanja, SunSport lilibaini kuwa klabu hiyo ina mpango wa kumsajili Neymar na mpango wao umeishitua Barcelona, kwa mujibu wa taarifa kutoka Catalonia.

Jose Mourinho anataka kusajili nyota mwenye jina kubwa kuongeza nguvu katika kikosi cha Mashetani Wekundu ili irudi katika kiango chake.

Gazeti hilo la England lilidai kuwa Man United imekutana na wakala wa Neymar na ipo tayari kumpa ofa nono nahodha huyo wa Brazil kwa mshahara wa Pauni 416,000 kwa wiki baada ya kodi.

Mabingwa wa England mara 20 wapo tayari kumfanya nyota huyo kuwa bora zaidi na kuneemeka mara mbili ya alivyo katika klabu ya Barcelona, wakinunua mkataba wake kwa Pauni 173 milioni.