Mourinho kupigwa kalamu

Saturday October 31 2015

JOSE MOURINHO: Ana uhakika wa kubadili mambo

JOSE MOURINHO: Ana uhakika wa kubadili mambo katika kikosi baada ya wachezaji kudai watampa sapoti. 

KARATA ya mwisho kwa Jose Mourinho. Hakuna namna nyingine zaidi ya ushindi tu ndio utakaokinusuru kibarua chake klabuni Chelsea.

Mourinho ataiongoza Chelsea kwenye mchezo mgumu wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool uwanjani Stamford Bridge leo Jumamosi na kwamba ushindi tu ndiyo utakaokinusuru kibarua chake baada ya timu hiyo kukumbana na vichapo vitano katika mechi 10 ilizocheza hadi sasa kwenye ligi hiyo.

Chelsea inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo baada ya kuvuna pointi 11 tu, huku ikiwa imeshinda mechi tatu na kutoka sare mbili, takwimu zinazothibitisha kiwango duni kwa mabingwa hao watetezi.

Mourinho anategemea rekodi nzuri dhidi ya Liverpool ambapo katika mechi sita za karibuni, Chelsea imeshinda mara tatu na kutoka sare tatu, lakini sasa pale Anfield kuna kocha mpya, Jurgen Klopp, ambaye pia anahitaji kupata ushindi ili kuweka mambo sawa baada ya kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Brendan Rodgers. Klopp amepoteza mechi moja tu kati ya nne alizocheza dhidi ya Mourinho. Mourinho akikubali kichapo tu, imekula kwake.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo, Arsenal ambayo imekabana kwa pointi na vinara Manchester City itakuwa ugenini kwa Swansea City, ambao msimu huu imekuwa moto kweli kweli kwenye safu yao ya ushambuliaji baada ya kombinesheni nzuri inayoundwa na Bafetimbi Gomis na Andre Ayew.

Lakini, Arsenal itaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya kufunga mabao 1,999 tangu ilipoanza kuwa chini ya Kocha Arsene Wenger, hivyo itahitaji kufunga zaidi.

Man City itakuwa nyumbani Etihad kucheza dhidi ya Norwich City, huku Manchester United ikienda ugenini kwa Crystal Palace, ikiwa na kazi moja kusaka bao la kwanza baada ya kucheza mechi mbili zilizopita bila ya kufunga.

Mechi nyingine za leo, West Brom itakipiga na Leicester City, ambayo kwa sasa inatambia straika wake Jamie Vardy, Watford itacheza na West Ham, Newcastle itakipiga na Stoke City, wakati kesho Jumapili, Everton itakuwa na kazi ngumu mbele ya Sunderland na Southampton itamaliza ubishi na Bournemouth.

Usiku wa Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja, ambapo Tottenham itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa White Hart-Lane kucheza na Aston Villa.