Mourinho aongeza utata kwa mwamuzi

Muktasari:

  • Mourinho anadai kwamba ana wasiwasi mpuliza filimbi huyo anapewa presha kubwa na mashabiki wa Liverpool kwa makusudi na kuna uwezekano akachanganyikiwa wakati wa mechi na kutoa maamuzi ya mabovu kutokana na shinikizo la mashabiki hao. Mashabiki wa Liverpool hawaamini kama mwamuzi huyo ameteuliwa kuchezesha mechi hiyo ya mahasimu wa England huku akiwa anaishi maili sita tu kutoka katika uwanja wa Manchester United katika eneo linaloitwa Altrincham.

LIVERPOOL, ENGLAND. SIKU ya shughuli ishafika, ni Liverpool dhidi ya Manchester United, mechi itachezwa usiku, lakini kabla hatujafika usiku tutasikia mengi.

Na kwa sasa anayeongoza kwa kuongelewa katika mechi ya leo ni Mwamuzi, Anthony Taylor ambaye bado uteuzi wake umejaa utata.

Mwanzoni ilionekana kama Liverpool walikuwa wanajihami na uteuzi wa mwamuzi huyo anayeishi Jiji la Manchester, lakini safari hii Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho naye amegundua janja ya nyani ameanza kujihami pia.

Mourinho anadai kwamba ana wasiwasi mpuliza filimbi huyo anapewa presha kubwa na mashabiki wa Liverpool kwa makusudi na kuna uwezekano akachanganyikiwa wakati wa mechi na kutoa maamuzi ya mabovu kutokana na shinikizo la mashabiki hao. Mashabiki wa Liverpool hawaamini kama mwamuzi huyo ameteuliwa kuchezesha mechi hiyo ya mahasimu wa England huku akiwa anaishi maili sita tu kutoka katika uwanja wa Manchester United katika eneo linaloitwa Altrincham.

“Nadhani kuna mtu kwa makusudi kabisa anaweka presha kwake. Itakuwa vigumu kwake kuwa katika kiwango kizuri. Mr Taylor ni mwamuzi mzuri sana. Nina mtazamo wangu kuhusu suala hilo lakini sitaki kusema chochote kwa sababu nimejifunza baada ya kuadhibiwa sana huko nyuma,” alisema Mourinho.

Hata hivyo, licha ya kujihami huko, FA bado inaweza kumfungulia mashabiki kocha huyo Mreno kwa sababu kwa mujibu wa kanuni zao, makocha hawaruhusiwi kuongea lolote kuhusu waamuzi kabla ya mechi kuchezwa.

Inaonekana wazi kwamba Mourinho anaamini kuwa, Taylor anaweza kuathirika kisaikolojia na ulalamishi wa watu wa Liverpool kiasi kwamba anaweza kuinyonga United kwa ajili ya kuthibitisha kwamba anatenda haki katika mechi hiyo.

United pia inaamini kuwa utata juu ya mwamuzi huyo ungeweza kuepukwa tu kwa kumchagua mwamuzi ambaye haishi karibu na Old Trafford. Hilo lingeweza kufanyika kwa kumchagua mwamuzi mahiri, Mark Clattenburg ambaye hajachezesha pambano lolote wikiendi hii. Clattenburg amechezesha mechi nyingi kubwa ambapo Mei mwaka huu alichezesha pambano la fainali za Ulaya kati ya Real Madrid na Atletico Madrid katika dimba la San Siro huku akilimudu vema pambano hilo la watani wa jadi.

Lakini mwezi uliofuata mwamuzi huyo ambaye ni shabiki mkubwa wa Newcastle ambaye hachezeshi mechi za timu hiyo alichezesha pambano la fainali za Euro 2016 kati ya wenyeji Ufaransa dhidi ya Ureno ambao walishinda mechi hiyo kwa bao 1-0 na kutwaa taji hilo. Clattenburg pia alichezesha pambano la fainali za Kombe la Ligi mwaka huu kati ya Crystal Palace dhidi ya Manchester United ambalo lilikwenda hadi katika dakika za nyongeza huku United ikishinda mabao 2-1.

Kwa jumla, rekodi ya Taylor kwa Liverpool ni mbovu huku akiwa amewapa Liverpool kadi nyingi za njano kuliko maadui zao katika mechi zote alizowachezesha Ligi Kuu ya England, huku pia akiwa amewapa kadi nyekundu mara mbili.

Kuchochea ugumu wa takwimu zake, mwamuzi huyo hajawahi kuwaonyesha United kadi yoyote nyekundu huku akiwa amewapa idadi chache ya kadi za njano kitu ambacho kinawapa wasiwasi mashabiki wa Liverpool ambao wameonyeshwa kushtushwa na uteuzi wake.Uteuzi wa waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu ya England unafanywa na kampuni ya waamuzi wa kulipwa (PGMOL) na tayari uamuzi wa kumteua Taylor umepondwa vibaya na mwamuzi wa zamani wa Ligi Kuu ya England, Mark Hasley. “PGMOL wanajiweka katika wakati mgumu. Kama kitu chochote kikitokea kutakuwa na maswali” alisema Halsey.