Mourinho analialia

Friday February 17 2017

MANCHESTER, ENGLAND. JOSE Mourinho amekiri kwamba mastaa wake wa Manchester United watakuwa na wakati mgumu kama watasonga mbele kwenye michuano ya Europa League na Kombe la FA.

Man United kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini watakuwa na mechi dhidi ya Southampton kwenye fainali ya Kombe la Ligi baadaye mwezi huu na hapo watakuwa na mechi ya Kombe la FA na Europa League pia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mechi yake ya kwanza dhidi ya Saint-Etienne iliyotarajiwa kufanyika usiku wa jana uwanjani Old Trafford, Mourinho alisema anawaza sana kuhusu ratiba itakavyokuwa ngumu na kuwabana.

“Hapa Manchester United hatuchagui michuano. Tunafahamu hali yetu ni ngumu, tuna mechi za Europa League, Kombe la FA, Kombe la Ligi na mechi za ligi nyingine zimeahirishwa, hivyo tutakuwa kwenye wakati mgumu tukisonga mbele kwenye michuano yote hiyo na hapo kuna majeruhi,” alisema Mourinho.

“Tunacheza kila michuano ili kushinda na nadhani pia ni muhimu kuwapa wachezaji uzoefu. Europa League tunayoitaka kucheza,  tutaipa heshima. Lakini, ukiangalia ratiba ni ngumu kuna mechi dhidi ya Manchester City imeahirishwa.

“Kama tutashinda dhidi ya Blackburn mechi na Southampton itaahirishwa pia kwa sababu robo fainali inachezwa kwenye wiki ambazo Ligi Kuu ilipaswa kuchezwa. Unaona inavyokwenda kutuweka kwenye wakati mgumu.”

Mchezo ujao Ligi Kuu England itakipiga na Bournemouth, Machi 4.