KHAA BALAA : Mourinho aamua kumpa Zlatan likizo

Zlatan Ibrahimovic.

Muktasari:

  • Mourinho amempa likizo mshambuliaji huyo mrefu na hatakuwepo katika pambano la leo usiku michuano ya Europa dhidi ya Zorya Luhansk ya Ukraine na staa huyo amepaa mpaka Milan kwa ajili ya kula bata.

Manchester,England. KUMTUNZA mwanasoka mwenye miaka 34 inahitaji akili ya ziada. Ndicho anachojaribu kukifanya Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho kwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic.

Mourinho amempa likizo mshambuliaji huyo mrefu na hatakuwepo katika pambano la leo usiku michuano ya Europa dhidi ya Zorya Luhansk ya Ukraine na staa huyo amepaa mpaka Milan kwa ajili ya kula bata.

Staa huyo alionekana akizurura katika mitaa ya Milan huku pia akila chakula cha usiku katika Mgahawa wa Finger’s Garden ambao unamilikiwa na staa wa zamani wa AC Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Clarence Seedorf ambaye aliwahi kucheza naye Milan.

Zlatan ameibeba United tangu alipotua akitokea PSG kwa uhamisho huru katika dirisha kubwa la majira ya joto lililopita huku akiingia mkataba wa mwaka mmoja tu na anachukua dau la Pauni 200,000 kwa wiki.

Zlatan alisifiwa sana na Mourinho kwa mchango wake alioutoa katika pambano dhidi ya Leicester City Jumamosi iliyopita na ingawa hakufunga lakini alipiga soka safi huku United ikiizamisha Leicester mabao 4-1.

Katika mechi zote tano zilizopita, Zlatan amecheza dakika 90 kila mechi mpaka sasa na Mourinho ameamua kumpumzisha kwa ajili ya kulinda nguvu zake huku United ikiwa inashiriki katika michuano mingi ambayo inataka kufanya vizuri.

United inashiriki katika Ligi Kuu ya England, michuano ya Europa, Kombe la Ligi na FA.

Kutokana na Zlatan kupewa likizo, Mourinho leo anatazamiwa kumchezesha kiungo mahiri mchezeshaji wa kimataifa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan ambaye alitolewa wakati wa mapumziko katika pambano dhidi ya Manchester City.

Kabla ya hapo Mkhitaryan (27), alikosa mechi nne zilizopita kutokana na kuwa na majeraha ya paja na mashabiki wa United wamekuwa na hamu kubwa ya kuona kipaji cha staa huyo ambaye aliondoka Ujerumani akiwa na rekodi nzuri.

Mkhitaryan alinunuliwa kwa dau la Pauni 36 milioni akitokea Borussia Dortmund na nafasi yake imekuwa ikichezwa na nahodha, Wayne Rooney ambaye hata hivyo naye aliwekwa benchi katika pambano dhidi ya Leicester City.

Hii ina maana kwamba Rooney na Mkhitaryan watacheza namba tisa na namba 10 leo na hii ni nafasi yao kubwa kuthibitisha uwezo wao kwa ajili ya kumshawishi kocha huyo ambaye siku za karibuni alikuwa katika kitimoto.

United inalazimika kupambana kufa na kupona kushinda pambano la leo baada ya kupoteza katika pambano la kwanza dhidi ya Fayenoord ya Uholanzi kwa kuchapwa bao 1-0 jijini Rotterdam wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa Kocha Mourinho haichukulii kwa umuhimu michuano hiyo na akili yake kubwa ameielekeza katika kuirudisha United katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ambayo United imeikosa baada kushika nafasi ya tano chini ya Kocha, Louis van Gaal aliyetimuliwa Mei mwaka huu.