PESA KWELI INAONGEA: Man City yafunika 2016, Arsenal namba nne

Muktasari:

  • Kwa taarifa tu, Manchester City ndio timu iliyotumia pesa nyingi zaidi kuliko nyingine, huku Hull City ikiwa imetumia pesa ndogo zaidi

LONDON, ENGLAND. MWAKA 2016 umebakiza saa zisizozidi 48 kufika mwisho na kuanza Mwaka Mpya 2017.

Makocha wa Ligi Kuu England watakaribisha Mwaka Mpya kwa kufanya usajili ili kuboresha vikosi vyao, huku wengine wakitarajia kuwa na mapengo kutokana na baadhi ya nyota wao wa Kiafrika kurudi Afrika kuungana na timu zao za taifa kwa ajili ya michuano ya Afcon itakayofanyika huko Gabon.

Hata hivyo, swali la kimichezo linalosumbua mashabiki kwa sasa ni juu ya ufahamu ni timu gani zilizopo kwenye Ligi Kuu England ilitumia pesa nyingi kwenye usajili kuliko nyingine kwa mwaka 2016?

Dirisha la uhamisho wa wachezaji wa mwezi Januari na lile la kipindi cha majira ya kiangazi, klabu za England zilitumia pesa karibu Pauni 1.2 bilioni kwa usajili wa mastaa mbalimbali kutoka kona mbalimbali za dunia hii.

Kwa taarifa tu, Manchester City ndio timu iliyotumia pesa nyingi zaidi kuliko nyingine, huku Hull City ikiwa imetumia pesa ndogo zaidi, kwani pesa iliyotumia kwenye usajili wa mastaa mbalimbali wa timu hiyo, hata kumsajili Marouane Fellaini peke yake haitoshi.

Man City imetumia zaidi ya Pauni 174 milioni katika kuwasajili John Stones (Pauni 50 milioni), Leroy Sane (Pauni 37 milioni), Gabriel Jesus (Pauni 27 milioni), Ilkay Gundogan (Pauni 21 milioni), Claudio Bravo (Pauni 17.1 milioni), Nolito (Pauni 13.8 milioni), Marlos Moreno (Pauni 4.75 milioni) na Oleksandr Zinchenko (Pauni 3.4 milioni).

Majirani zao, Manchester United wamezidiwa Pauni 25 milioni tu baada ya kufanya usajili mkubwa wa Pauni 89 milioni kumnasa Paul Pogba na kisha kuwasajili Eric Bailly (Pauni 30 milioni) na Henrikh Mkhitaryan (Pauni 26.3 milioni.)

Chelsea inashika namba tatu kwa matumizi ya wachezaji kwa mwaka wote wa 2016 baada ya kutumia zaidi ya Pauni 100 milioni kwa kuwasajili Michy Batshuayi (Pauni 33.2 milioni), N’Golo Kante (Pauni 32 milioni), David Luiz (Pauni 30 milioni) na Marcos Alonso (Pauni 23 milioni).

Arsenal ipo kwenye nne bora kwa kutumia Pauni 93.1 milioni na mabingwa watetezi, Leicester City wanakamilisha Tano Bora kwa kutumia 76 milioni, wakiizidi Liverpool, ambayo imetumia Pauni 75 milioni katika manunuzi ya wachezaji kwa mwaka 2016.

Matumizi ya timu nyingine, ndani ya 10 bora ya zilizomwaga pesa kwenye usajili, zipo Watford iliyosajili kwa Pauni 72.1 milioni, Tottenham Hotspur (Pauni 70.6 milioni), Everton (Pauni 65 milioni) na AFC Bournemouth (Pauni 56.6 milioni).

Kwenye 10 la mwisho linalokamilisha idadi ya timu zilizopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Crystal Palace imetumia Pauni 56.5 milioni, Southampton (Pauni 47.8 milioni), West Ham United (Pauni 47.35 milioni), Sunderland (Pauni 41.85 milioni), Stoke City (Pauni 36.55 milioni), Swansea City (Pauni 35.25 milioni), Middlesbrough (Pauni 27.8 milioni), West Bromwich Albion (Pauni 22.5 milioni), Burnley (Pauni 22.1 milioni) na timu inayoshika mkia kwenye ligi hiyo ya utumiaji wa pesa ni Hull City, iliyotumia Pauni 19.5 milioni.