MDOMO WAZI : Bailly apagawisha Man United

Muktasari:

  • Ander Herrera, Michael Carrick na Luke Shaw wamepiga saluti kwa kiwango kilichoonyeshwa na mlinzi, Eric Bailly tangu kuwasili klabuni hapo huku wakidai mlinzi huyo ni ‘Mnyama’ na ‘Mlinzi wa kweli’.

Manchester,England. NDIYO, mdomo wazi. Wamepigwa na mshangao. Wachezaji wa Manchester United walidhani klabu yao imepoteza pesa kutoa Pauni 36 milioni kumnunua mlinzi mmoja wa Kiafrika katika Ligi Kuu Hispania lakini sasa wamenyoosha mikono juu.

Ander Herrera, Michael Carrick na Luke Shaw wamepiga saluti kwa kiwango kilichoonyeshwa na mlinzi, Eric Bailly tangu kuwasili klabuni hapo huku wakidai mlinzi huyo ni ‘Mnyama’ na ‘Mlinzi wa kweli’.

Bailly (22), alikuwa mchezaji wa kwanza kununuliwa na Kocha Jose Mourinho akitokea katika klabu ya Villarreal mnamo Juni 8 mwaka huu. Hata hivyo, jina lake halikuwa kubwa kwa mashabiki wa Man United pamoja na wachezaji wenzake.

Hata hivyo, nyota huyo alianza kuonyesha makali kwa kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi katika pambano la Ngao ya Hisani dhidi Leicester City kabla ya kucheza soka la hali ya juu katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu dhidi ya Bournemouth na Southampton.

Sasa, Ander Herrera, Michael Carrick na Luke Shaw ambao walikuwepo klabuni hapo kumpokeas Bailly wameeleza kushangazwa na kiwango cha nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.

“Nadhani Eric ana kipaji kikubwa sana. Ni mnyama. Ana nguvu, mwepesi na ni mchezaji mwenye akili. Hapendi kuhatarisha mpira kwa hiyo ni muhimu kwamba wakati tuna mpira au ana mpira, tunajua hawezi kuiweka timu katika matatizo,” alisema Herrera.

“Wakati adui anapokuwa na mpira tunajua kuwa tuna mchezaji mwepesi, tunaweza kukabia juu kwa sababu tunajua Eric ataziba nafasi zetu. Ni mzuri sana hewani, ana nguvu, mpira wowote wa kuwaniwa anakwenda kama mwendawazimu na anaupata. Alifanya vizuri alipocheza na Jamie Vardy na haikuwa kazi rahisi kwa sababu Vardy alikuwa mmoja kati ya wachezaji bora msimu uliopita lakini Bailly aliupata kila mpira wa juu,” alisema Herrera.

“Tuna furaha naye sana. Huu msimu ni mrefu kwa hiyo inabidi tutulie sana na Eric atakuwa muhimu sana kwetu ingawa bado ni mdogo na anahitaji kuimarika zaidi.”

Naye Carrick, ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wakongwe klabuni hapo ameelezea kukoshwa na kiwango cha Bailly huku akitoa ushuhuda kuwa ni mlinzi wa nguvu ambaye Man United walikuwa wanamhitaji kwa ajili ya kurudisha heshima yao.

“Eric anaonekana kufurahia kukaba. Siku hizi siyo kitu cha kawaida sana, naona walinzi wengi wanapenda sana kuchezea mpira. Eric ni mlinzi wa kweli. Alicheza vizuri sana Wembley na nina uhakika kila siku atakuwa anaimarika.”

Naye Shaw ambaye ameanza mechi zote tatu za msimu huu kuanzia pambano dhidi ya Leicester akicheza sambamba na Bailly amesema mlinzi huyo ni aina ya mabeki ambao Manchester United inawahitaji kwa sasa.

“Yeye ndiye aina ya mchezaji tunayemhitaji. Anatulia na mpira na katika wakati mwafaka anajua ni muda gani wa kuuondoa au kucheza kuanzia nyuma.

Katika safu ya ulinzi amekuwa mgumu sana na hakuna aliyempita na ndiyo maana tuna furaha kuwa naye hapa. Ni mchezaji mzuri sana na katika mechi chache tu alizocheza ameonyesha jinsi alivyokuwa muhimu kwetu,” alisema Shaw.

Eric Bertrand Bailly alizaliwa Aprili 12, 1994 Bingerville nchini Ivory Coast na alianza maisha yake ya soka la kulipwa katika klabu ya Espanyol kabla ya kuhamia klabu ya Villarreal kwa dau la Euro 5.7 milioni 2015. Ameichezea timu hiyo kwa msimu mmoja tu kabla ya kutua United katika dirisha hili. Alikuwepo katika kikosi cha Ivory Coast ambacho kilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka jana.