Liverpool imelamba dume kumnasa Klopp

Friday October 9 2015

Sasa tunaanza kazi. Mimi sio mtu wa ndoto

Sasa tunaanza kazi. Mimi sio mtu wa ndoto ndoto, simtaki Cristiano wala Lionel. Nakitaka kikosi hiki hiki, ni uamuzi wao vijana, tunaanza kazi. Klopp 

LONDON, ENGLAND

MAKAO makuu ya Liverpool, Melwood jana yalitazamiwa kumpokea mgeni maarufu, Jurgen Klopp ambaye anatazamiwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo baada ya Brendan Rodgers kutimuliwa Jumapili. Lakini mgeni huyo ameanza kupokea sifa nyingi kutoka kwa watu wanaomfahamu.

Kiungo wa zamani wa Liverpool, Dietmar Hamann na beki wa Borussia Dortmund, Mats Hummels wamekiri kwamba Liverpool imefanikiwa kulamba dume kwa kumnasa kocha huyo Mjerumani aliyeifundisha Dortmund kwa mafanikio makubwa.

“Atajichanganya nao, atajaribu kuwa mmoja wao na ndiyo maana naona watakuwa washkaji sana kati yake na mashabiki. Ni uteuzi mzuri sana, ni wazi kwamba ni chaguo langu kwa kocha haswa anayetakiwa kuwa wa Liverpool kwa sababu anapenda sana soka na atafiti nao vizuri sana,” alisema Hamann.

“Ni muda mwafaka kuwa kocha wa Liverpool kwa sababu katika kipindi cha miaka tisa au 10 wana Kombe la Ligi tu. Wamecheza msimu mmoja tu katika Ligi ya Mabingwa kati ya misimu sita iliyopita na ni wazi kwamba mambo hayajawa mazuri kwa kweli.”

“Inabidi utengeneze hisia kwa mashabiki tena na hiyo ni sehemu kubwa ya Liverpool, ni sehemu kubwa kwa staili ya menejimenti na nadhani atafaa sana,” aliongeza Hamann ambaye aliichezea Liverpool kuanzia mwaka 1999 mpaka 2006.

Alipoulizwa kama falsafa za ukocha za Klopp zitaendana na Liverpool, Hamann alijibu: “Anapenda kucheza soka la nguvu akitumia timu yenye damu changa. Hiyo ndiyo ilikuwa staili yake na ndivyo alivyokuwa akiichezesha Borussia Dortmund, klabu ambayo aliibadili kwa miaka kadhaa.”

“Klopp anataka kuingiza wachezaji vijana, huwa hajali kufanya kazi na wachezaji chipukizi. Baadhi ya wachezaji aliowaleta Dortmund wamekuwa vipaji halisi na wamekuwa miongoni mwa wachezaji bora dunani. Aliwageuza wachezaji wa kawaida wasiojulikana kuwa wachezaji wa hadhi ya dunia. Kwa hiyo kombinesheni ya vitu hivi viwili itakuwa nzuri. Nadhani atakuwa kocha mwenye mafanikio.”

Wakati Hamman akimnadi kocha huyo kwa kauli hizo, Hummels ambaye ni nahodha wa Dortmund na alipewa kazi hiyo na Klopp wakati akiwa kocha wa timu hiyo alidai kwamba Liverpool imenasa dume kwa kufanikiwa kumpatia mkataba kocha huyo.

“Hakuna shaka kwamba ni bonge la kocha. Ni kocha mzuri. Wakati watu walipokuwa wanaulizana ni kitu gani ambacho angekwenda kufanya baada ya kuondoka Dortmund, Liverpool iliingia katika mipango. Anaishi, anapumua, anafikiria kuhusu soka kila siku. Ni chaguo zuri kwa timu yoyote ile na nasubiri kwa hamu kuona maendeleo yake katika hatua nyingine ya ukocha wake,” alisema Hummels.

Mkongwe wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Franz Beckenbauer ambaye alifanya kazi ya uchambuzi katika kituo cha Ujerumani na Klopp alidai kwamba Liverpool itakuwa imefanikiwa kumnasa bonge la kocha kama ikimpata Klopp.

“Ni bonge la kocha. Ni mmoja kati ya makocha bora ninaowajua duniani na alifanya mambo makubwa akiwa na Borussia Dortmund. Aliichukua klabu ya kawaida na kuifanya kuwa klabu bora duniani. Kama Liverpool ina nafasi ya kumnasa Jurgen Klopp, inabidi ifanye hivyo. Anapenda kuongea. Hakuna makocha wengi duniani waliobaki ambao wanapenda sana kuongea na wachezaji lakini yeye ni mmoja wao.”

Klopp anatarajiwa kutua Anfield na wasaidizi wake wawili aliowahi kufanya nao kazi Dortmund ambao ni Zeljko Buvac, pamoja na mchambuzi wake wa mechi Peter Krawietz. Anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu na anatarajiwa kulipwa zaidi ya dau la Pauni 3.6 milioni kwa mwaka ambalo alikuwa akichukua Dortmund.