Kwa Wenger mtangoja sana! Hang’atuki

Monday February 13 2017

 

LONDON, ENGLAND. ARSENE Wenger amekuwa king’ang’anizi baada ya kusisitiza kwamba hayupo tayari kung’atuka Arsenal.

Staa wa zamani wa Arsenal, Ian Wright alidai Wenger amechoka  baada ya kudumu kwa zaidi ya miaka 20 katika kikosi hicho na kwamba muda wake umepitwa na wakati, kitu ambacho bosi huyo Mfaransa amekuja juu na kumjibu kwamba kama wanataka akapumzike, muda wake bado wa kufanya hivyo.

Wenger alidai hilo baada ya kushuhudia kikosi chake kikiichapa Hull City 2-0 juzi Jumamosi, wakati yeye akiwa jukwaani kutokana na kutumikia adhabu.

Wenger (67) alisema: “Sipo tayari kupumzika. Hatuzungumzii mambo binafsi na sipo tayari kuonyesha mambo yangu ya baadaye.”

Hata hivyo, wakati Wenger akikomaa kwamba haondoki Arsenal, ripoti zimefichuka huko Emirates kwamba Rafa Benitez sasa anakuja kuchukua mikoba yake na kwamba Thierry Henry ataungana naye kuwa kocha msaidizi.

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa kukitajwa makocha mbalimbali wanaohusishwa na kiti hicho cha Wenger klabuni Arsenal na habari mpya ni kuhusu Kocha wa Newcastle United, Benitez.

Makocha wengine waliohusishwa na kiti hicho cha kuinoa Arsenal ni Thomas Tuchel wa Borussia Dortmund, Luis Enrique wa Barcelona na Leonardo Jardim wa Monaco.

Kuhusu Henry, tayari ameshaonja majukumu ya ukocha baada ya kuwa na Roberto Martinez katika kikosi cha Ubelgiji.

Wenger amedumu kwenye kikosi cha Arsenal kwa miaka 21, lakini kwa kipindi cha karibuni ameripotiwa kuibua mgawanyiko kwa mashabiki ambapo kuna makundi mawili, moja linamsapoti na jingine linataka aondoke baada ya kikosi hicho kusubiri kwa miaka 12 kubeba taji la Ligi Kuu England na kwamba huu unaweza kuwa mwaka wao wa 13 wakiendelea kusubiri taji hilo bila mafanikio.