Klopp: Kama Madrid, Man U haziiwezi Bayern nani ataweza?

Muktasari:

  • Klopp (46), ambaye msimu uliopita aliitambia Real Madrid kwenye nusu fainali kwa kuwashinda jumla ya mabao 4-3, kwenye fainali alimenyana na Bayern Munich na kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 uwanjani Wembley.

MUNICH, UJERUMANI

KOCHA wa Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amesema kama Real Madrid na Manchester United hazionekani kufikiriwa kama zitaweza kuifunga Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi hakuna timu nyingine itakayoiweza timu hiyo msimu huu.

Klopp (46), ambaye msimu uliopita aliitambia Real Madrid kwenye nusu fainali kwa kuwashinda jumla ya mabao 4-3, kwenye fainali alimenyana na Bayern Munich na kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 uwanjani Wembley.

Msimu huu, Bayern Munich ikionekana kuwa kwenye ubora mkubwa zaidi tangu ilipokuwa chini ya kocha Pep Guardiola, Klopp alisema anadhani timu hiyo kwa sasa haifungiki.

“Hata Real Madrid hawaiwezi Bayern Munich,” alisema Klopp alipokaririwa na gazeti la A Bola.

“Bayern hii ya sasa haishikiki. Kama timu za Real Madrid na Manchester United hazionekani kuwa na uwezo wa kuishinda timu hiyo, nani mwingine ataweza. Hata sisi Dortmund hatuwawezi.”

Klopp na kikosi chake cha Dortmund kwa sasa kimeachwa kwa pointi 12 na Bayern Munich kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga baada ya kucheza mechi moja zaidi. Kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya mtoano, Bayern Munich imepangwa kumenyana na Arsenal.