Kama zari!

Muktasari:

“Mwanzoni kabla ya mchezo, nilitabiri tutashinda. Nitaendelea kucheza na kufurahia ninachokifanya hapa England.”

LONDON, ENGLAND. Lilikuwa bonge la bao alilofunga kwa kichwa na kurudisha tabasamu la Mourinho. Mechi hiyo ya fainali ya Kombe la Ligi, EFL, ilifanyika kwenye Uwanja wa Wembley.

Akizungumza na Sky Sports, Ibrahimovic, alisema:  “Hizi ni jitihada za timu. Hiki ndicho kilichonileta hapa England, kushinda na ninashinda. Kwa jinsi ninavyoshinda, ndivyo ninavyopenda iwe.

“Mimi ni mtu wa mataji, kila ninapokwenda mambo yanakuwa mazuri . Ninadhani hiki ni kikombe cha 32 kwangu.

“Mwanzoni kabla ya mchezo, nilitabiri tutashinda. Nitaendelea kucheza na kufurahia ninachokifanya hapa England.”

Ibrahimovic ndiye alianza kuifungia Manchester United bao la kuongoza kwa mpira wa frikiki kabla ya Jesse Lingard kufanya matokeo kusomeka 2-0. Lingard alifunga akiwa kwenye mazingira magumu baada ya kazi nzuri ya Marcos Rojo.

Southampton ilishambulia kwa nguvu kabla ya, Manolo Gabbiadini kupiga mpira uliompita tobo kipa wa Manchester United, David de Gea na Gabbiadini, aliyenunuliwa kwa dau la Pauni14m kutoka Napoli kusawazisha kwa shuti hafifu, na ndipo Ibrahimovic alipopiga mpira kichwa cha nguvu akiunganisha krosi ya Ander Herrera.

Ushindi huo unamfanya Mourinho kutwaa kikombe cha kwanza akiwa kocha wa Manchester United.

LA LIGA

Hispania. Lionel Messi aliifungia bao Barcelona dakika za mwishomwisho dhidi ya Atletico Madrid na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali wa Ligi kuu ya Hispania, Rafinha alianza kuifungia Barcelona bao la kwanza baada ya kazi nzuri ya Luis Suarez.

Hata hivyo, bao la Rafinha lilifutwa na  Diego Godin aliyeisawazishia Atletico akiunganisha kwa kichwa frikiki ya Koke.

Matokeo mengine, Espanyol ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Osasuna huku Athletic Bilbao ikitoka sare ya 1-1 na Granada.