Jose: Pogba? Subiri msimu ujao mtajua vizuri

MANCHESTER, ENGLAND. JOSE Mourinho amewaambia mashabiki wa Manchester United wasitake haraka vitu vitamu vya kiungo wao ghali, Paul Pogba na kwamba staa huyo Mfaransa atakuwa mtamu zaidi kuanzia msimu ujao.

Mourinho amesisitiza kwamba Pogba ndiye mchezaji atakayekuja kuwanyang’anya ufalme mastaa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kwenye tuzo ya Ballon d’Or.

Kocha huyo Mreno ameweka wazi pia kwa mabosi wa Man United kwamba hana lengo wala hafikirii kuwaruhusu mshambuliaji wake yeyote iwe Anthony Martial au Marcus Rashford kuondoka kwa mkopo katika dirisha lijalo la usajili litakalofunguliwa mwezi ujao.

Pogba sasa anaonekana kuanza kucheza kwa kiwango kizuri baada ya kuanza maisha yake ya Old Trafford vibaya kutokana na usajili wake wa pesa nyingi ulioweka rekodi ya uhamisho duniani wa Pauni 89 milioni akitokea Juventus kwenye dirisha lililopita.

Kwa wiki za karibuni, Pogba ameifanya Man United kuwa tamu ndani ya uwanja akiwa amepiga asisti nne katika mechi saba zilizopita na pasi zake zote hizo alimpigia Zlatan Ibrahimovic.

Hata hivyo, Mourinho anasema Pogba atakuwa mtamu zaidi na kila mtu atampenda kuanzia msimu ujao na atakachokifanya msimu huu ni kuboresha tu kiwango na kujiweka sawa kwa maandalizi hayo ya msimu ujao.

“Ligi Kuu England ni ngumu sana,” alisema Mourinho.

“Unaweza kucheza miaka mitatu au minne Italia, lakini ukija England unakutana na dunia tofauti kabisa. Anafanya vizuri, anafanya zaidi ya vizuri. Mabadiliko yake yanaonekana wazi. Naweza kuona msimu ujao, Paul atakuwa juu sana.”

Tuzo ya Ballon d’Or imekuwa ni kitu cha kugawana tu kati ya Ronaldo na Messi kwa takribani miaka tisa sasa, lakini Mourinho anaamini Pogba atakwenda kutibua hilo na atainyakua tu.

“Kwa sasa, kama si mfungaji wa mabao, huwezi kushinda Ballon d’Or,” alisema Mourinho.

“Lakini, kama mtazamo huo utabadilika, hapo Paul atashinda kwa sababu Paul si mfungaji. Paul ni kiungo ambaye atafunga tu mabao kwa sababu anafahamu namna ya kufunga. Kwa mtazamo wangu nadhani ni mchezaji bora duniani. Bado kijana, hivyo ana muda wa kuboresha zaidi kipaji chake. Siku zote anataka kuwa juu na hilo ni jambo zuri.”