JUMBA BOVU: Mourinho amshushia mzigo wa lawama Luke Shaw

Muktasari:

Man United juzi ilichapwa mabao 3-1 na Watford katika uwanja wa ugenini Vicarage Road ikiwa ni kichapo cha pili mfululizo katika Ligi Kuu England baada ya kuchapwa na Manchester City wikiendi iliyopita huku pia kikiwa ni kichapo cha tatu mfululizo katika michuano yote baada yakuchapwa na Feyenoord michuano ya Europa Alhamisi.

HAKUNA msiba usio na sababu. Manchester United wameanza kushikana uchawi baada ya vichapo kuanza kuwaandama. Sasa, Jose Mourinho kama kawaida yake amemtafuta mtu wa kumwangushia lawama ndani ya timu na amempata.

Man United juzi ilichapwa mabao 3-1 na Watford katika uwanja wa ugenini Vicarage Road ikiwa ni kichapo cha pili mfululizo katika Ligi Kuu England baada ya kuchapwa na Manchester City wikiendi iliyopita huku pia kikiwa ni kichapo cha tatu mfululizo katika michuano yote baada yakuchapwa na Feyenoord michuano ya Europa Alhamisi.

Mourinho anaamini kwamba mlinzi wake wa kushoto, Luke Shaw ndiye chanzo cha kufungwa kwa Man United katika pambano la juzi la Watford pamoja na lile walilochapwa na watani wao Manchester City, 2-1 nyumbani Old Trafford.

“Bao la kwanza la Man City na la pili la Watford yanafanana kabisa, lile la City, (Aleksandar) Kolarov alikuwa na mpira katika wakati mgumu pembeni badala ya kwenda kumkaba aliachiwa nafasi. Hapa katika bao la pili, (Nordin) Amrabat alipokea mpira na mlinzi wetu wa kushoto (Shaw) alikuwa mbali naye kwa mita 25 badala ya mita 5, lakini hata kama ni mita 25 inabidi umkimbilie na kukaba, lakini bado tunasubiri tu,” alisema Mourinho.

“Hili ni suala la mbinu, pia ni akili ya mtu. Ni kitu ambacho huwezi kukifanyia kazi ndani ya wiki chache. Naweza kuvigawa hivi vipigo katika sababu tatu, kwanza ni makosa ya waamuzi ambayo yapo nje ya uwezo wangu. Hakuna ninachoweza kufanya katika hilo. Katika pambano dhidi ya Manchester City mliona kilichotokea katika dakika ya 55 (Kipa wa Man City, Claudio Bravo alivyomchezea rafu Wayne Rooney). Mmeona kilichotokea katika bao la kwanza leo (Dhidi ya Watford), pia bao la Feyenoord lilikuwa la kuotea. Pili kuna suala la bahati mbaya. Ni sehemu ya mchezo.”

“Kitu cha tatu ni kilicho ndani ya uwezo wangu ambacho ni kuimarisha timu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Vile vile ni kujaribu kuzuia makosa ya ulinzi. Nilijua nilikuwa na kazi kubwa,” aliongeza Mourinho.

??Kwa hiyo inabidi tuimarike bila shaka, kwa mchezaji mmoja mmoja na kitimu. Na hiyo ni kazi yangu. Bahati mbaya siwezi kuzuia makosa ya waamuzi,” alimaliza Mourinho.

Wakati kocha huyo Mreno akilalamika hivyo, mastaa wawili wa zamani wa timu ya taifa ya England, Paul Scholes aliyekipiga Manchester United na kiungo, Steve McManaman aliyekipiga Liverpool na Man City walidai kwamba kiwango cha United hakieleweki na kinashtua sana. “Nadhani Manchester United walikuwa ovyo kabisa. Sijui walichokuwa wanakifanya, kwa muda mrefu sana walikuwa kama wako chini ya Louis van Gaal, jinsi walivyocheza ilikuwa vile vile tu. Nisingeweza kukwambia nani atacheza mechi ijayo kama timu nzima ikiwa fiti. Hakuna aliyekuwa tofauti,” alisema McManaman. Naye Scholes aliongeza;“Kama unaongelea fomesheni na nani acheze wapi, ubora wa wao kuwa na mpira ulikuwa duni sana upande wa Manchester United. Hivi ndivyo walivyo kwa sasa. Hauna uhakika unachoweza kupata kutoka kwa wachezaji. Rashford ndiye mchezaji anayeng’ara. Hakuwa na mechi nzuri lakini alionekana kuwa tishio. Kwa upande wa kumiliki mpira Manchester United ilikuwa ovyo sana.”

United irudi uwanjani kesho Jumatano katika Kombe la Ligi dhidi ya Northampton na Jumamosi itakipiga na Leicester City kwenye EPL.