Huyu kipa kibonge hivi anawasubiri Arsenal

Muktasari:

Shaw anatazamiwa kupangwa kwenye kikosi cha Sutton kinachoshiriki ligi ya mchangani huko England ambapo atakuwa na shughuli pevu ya kuzuia mashuti ya wakali kama Theo Walcott, Alexis Sanchez na wengineo.

KIPA kibonge kuliko yeyote kwenye soka la Uingereza, Wayne Shaw amesema amejiandaa vyema kabisa kwa ajili ya kuwabania Arsenal wakati watakapokwenda uwanjani Gander Green Lane Jumatatu katika mechi yao ya Kombe la FA.

Shaw anatazamiwa kupangwa kwenye kikosi cha Sutton kinachoshiriki ligi ya mchangani huko England ambapo atakuwa na shughuli pevu ya kuzuia mashuti ya wakali kama Theo Walcott, Alexis Sanchez na wengineo.

Shaw, ambaye ana umri wa miaka 45 ni mzito sana, lakini kila siku amekuwa akisafiri kwa umbali wa maili 80 kutoka nyumbani kwake huko Southampton hadi kufika kwenye uwanja wa nyumbani wa klabu yake ya Sutton United, ambao watakuwa wenyeji wa Arsenal katika mechi hiyo ya raundi ya tano ya Kombe la FA.

Sutton iliziduwaza Cheltenham, Wimbledon na Leeds kwa matokeo ya kushangaza kwenye michuano hiyo na sasa wanataka waishangaze Arsenal pia.

Kipa Shaw, ambaye mara nyingi anakuwa kwenye kikosi cha akiba alisema sawa kwa sasa hali si shwari huko Arsenal, lakini jambo hilo bado haliwapi uhakika wa kushinda mechi yao.

Anachokiamini Shaw ni kwamba Arsenal hawatakuwa na furaha watakapoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya timu hiyo ya mchangani na hilo linaweza kuwa sababu ya wao kushinda.

“Nadhani watakuja uwanjani wakiwa wameshabadili kabisa na kwenda moja kwa moja kupasha misuli kabla ya mechi kuanza,” alisema Shaw.

“Arsenal wanajiona hawaguswi. Lakini, tukienda 0-0 hadi dakika ya tano, basi itakuwa vizuri kwetu. Hii ni kama vita ya David na Goliath.”