Huu mkwara wa Ibrahimovic hatari

Muktasari:

  • Ibrahimovic alikuwa wa kwanza kutua Old Trafford Julai Mosi kwa uhamisho wa bure na kusaini mkataba wa mwaka mmoja

MANCHESTER, ENGLAND

SUPASTAA, Zlatan Ibrahimovic imefichuka kwamba kumbe alimpiga mkwara wakala wake Mino Raiola kwamba akithubutu kumpeleka Paul Pogba kwenye timu nyingine na si Manchester United atamvunja miguu.

Raiola, ni wakala wa Ibra na kiungo huyo wa Ufaransa na katika dirisha la usajili lililopita la majira ya joto aliuzia Man United wachezaji watatu wa maana, Zlatan, Henrikh Mkhitaryan na Pogba na kuingiza faida karibu ya Pauni 40 milioni.

Ibrahimovic alikuwa wa kwanza kutua Old Trafford Julai Mosi kwa uhamisho wa bure na kusaini mkataba wa mwaka mmoja na baada ya hapo Man United iliingia kwenye mazungumzo na Raiola kwa muda mrefu kuhusu Pogba hasa baada ya kumnasa Mkhitaryan pia.

Baada ya dili la Pogba kuonekana kuchelewa huku klabu nyingine kama Real Madrid na Paris Saint-Germain kuonekana kumhitaji staa huyo, Ibra aliamua kumpiga mkwara Raiola kwa kumwambia ole wake Pogba aende timu nyingine na si Man United.

“Zlatan ni mtu muhimu sana kwangu,” alisema Raiola.

“Alikuwa wa kwanza kusaini Man United na kisha akanipigia simu na kuniambia, ‘ole wako Pogba aende kujiunga na timu nyingine, nitakuvunja miguu yako.’

Raiola kisha akamtetea staa wake aliyempiga bei kwenye pesa nyingi iliyovunja rekodi ya dunia akisema ni suala la muda tu na timu kuelewana baada ya hapo Pogba mtaanza kumtambua.