Hee! Wenger anajua ubingwa ni wake

LONDON, ENGLAND. KOCHA, Arsene Wenger amedai ana silaha za maangamizi ya kuifanya timu yake kubeba taji la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kusubiri kwa miaka 13.

Kocha huyo anaamini kikosi cha kwa msimu huu cha Arsenal kipo vizuri kuliko chochote alichowahi kuwa nacho tangu mwaka ule wa 2004, ambapo Arsenal ilicheza bila ya kupoteza mechi hata moja.

Arsenal imeshafunga mabao 48 msimu kabla ya mechi yao ya jana Jumapili, ikiwa ni zaidi ya mabao 11 ya kiwango walichofunga msimu uliopita walipokuwa wamecheza idadi kama hiyo ya mechi.

Wenger alisema: “Najua nina silaha za kutosha. Nadhani tumekuwa wagumu msimu huu, tunatisha zaidi. Ukitazama timu zilizofunga mabao mengi kwenye dakika tano za mwisho, sisi ndiyo wababe na wafungaji wengi pia wanaoanzia kwenye benchi. Hivyo tuna silaha za kutosha kwenye safu ya ushambuliaji.

“Kwenye benchi tunao Danny Welbeck, Lucas Perez, Olivier Giroud na Theo Walcott. Hawa ni wachezaji ambao muda wote unatarajia watakupa kitu.”

Arsenal jana ilitarajia kumenyana na Burnley katika mchezo wa Ligi Kuu England Uwanjani Emirates. Kocha huyo ana tamaa ya ubingwa ili kukata kiu ya mashabiki wake ambao wamekuwa wakimzonga kwa kukosa mbinu sahihi.