HII KALI: Sikia Mourinho anavyojitutumua

Monday September 14 2015

 

 LIVERPOOL, ENGLAND

INABIDI ajikaze kiume tu maana hakuna jinsi. Utafanyaje sasa? Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amelazimika kujikaza kiume baada ya kushuhudia timu yake ikichapwa mchezo mwingine tena kwa Ligi Kuu ya England juzi mchana.

Chelsea ilichapwa mabao 3-1 na Everton katika dimba la Goodson Park jijini Liverpool na hicho kinakuwa kipigo cha pili cha Chelsea ndani ya mechi tano tu za Ligi Kuu England baada ya kuchapwa na Manchester City 3-0 katika pambano la pili la msimu.

Kipigo hicho kimemwacha Mourinho na kikosi chake wakiwa na pointi 4 baada ya mechi tano na huo unakuwa mwanzo mbaya wa Ligi kwa Chelsea kwa kipindi cha miaka 29 iliyopita.

Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa, Mourinho ameibuka na kujikaza kiume.

“Mimi ni bingwa, wachezaji wangu ni mabingwa, kwa jinsi wanavyocheza si vibaya sana kama matokeo yanavyoonekana lakini katika kila mechi mambo yanakwenda vibaya kwetu. Inabidi tukubali kwa sababu soka ni mchezo wa matokeo.  Ni rahisi kusema na nakubali kabisa, lakini matokeo ni mabaya sana,” alisema Mourinho.

“Siwalaumu wachezaji wangu na wala sijilaumu mwenyewe. Sikubali matokeo, mimi nawajibika kwa timu, sina furaha na hali ilivyo na sina furaha na mwenyewe. Nipo na wachezaji, siwezi kuwa dhidi yao, siwezi kuwa na hisia mbaya na wao. Hilo ndilo linalonifanya niwe na furaha,” alisema Mourinho.

“Nina furaha kwamba kesho ninaenda kukutana nao tena mazoezini na kufanya mazoezi na wao kwa ajili ya kujiandaa na mechi ijayo,” aliongeza kocha huyo Mreno mwenye maneno mengi.

“Samahani, mpaka mtu achukue ubingwa, bado sisi ni mabingwa. Nimezoea vizuri. Sina presha. Wakimbizi wana presha kubwa. Matokeo ni mabaya zaidi kuwahi kuyapata. Sina furaha lakini naendelea kuizoea hii hali. Kipaumbele ni kuendelea kufanya kile ambacho tunafanya, wachezaji wanajisikia huzuni sana.”

“Hatustahili matokeo haya. Wasiwasi mkubwa ni kwamba kila kitu kinakwenda dhidi yetu. Tunafanya makosa na tunaadhibiwa hapo hapo. Mimi ndiye mtu wa kufanya kazi hii. Sidhani kama kuna mtu mwingine anayeweza kufanya kazi hii zaidi yangu. Kuhusu ubingwa? Sijui. Kwa sasa haupo mikononi mwetu.”

Kama vile haitoshi, Jumamosi ijayo Chelsea itakuwa na mtihani wakati itakapocheza na wapinzani wao wa jiji la London, Arsenal katika dimba la Stamford Bridge huku wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwao katika pambano la Ngao ya Jamii Agosti mwaka huu.

Na kuongeza presha kwa Mourinho timu zote tatu kubwa ambazo zinatazamiwa kumpa upinzani msimu huu, Manchester City, Arsenal na Manchester United zilishinda katika mechi zao za Jumamosi.

 Manchester City waliikandamiza Crystal Palace kwa bao la dakika za majeruhi la kinda wa Nigeria, Keleshi Ihenacho na hivyo kwenda kileleni wakiongoza ligi kwa pointi 15.

Wakati Manchester United waliwatandika wapinzani wao Liverpool kwa mabao 3-1 Uwanja wa Old Trafford.

 Arsenal waliichapa Stoke City 2-0 katika uwanja wa nyumbani Emirates na timu hizo mbili zimefikisha pointi 10 kila mmoja.