HATARI TUPU: Sergio Aguero hatihati kwa Manchester United

Muktasari:

  • City iliichapa West Ham mabao 3-1 katika Uwnaja wa Etihad, lakini kasheshe kubwa ilitokea katika dakika ya 76 ya pambano hilo wakati Aguero alipoonekana akimtwanga kiwiko cha koo Reid ambaye hakuweza kuendelea na pambano hilo na nafasi yake ikachukuliwa na Jonathan Calleri.

JOTO limeanza kupanda mapema na wasiwasi umeanza kuingi mapema zaidi. Pambano kubwa lijalo la Ligi Kuu ya England ni kati wababe wawili wa Jiji la Manchester kati ya Manchester United na Manchester City dimba la Old Trafford na tayari matukio yameanza kutokea.

Kuna wasiwasi mkubwa Manchester City ikamkosa mshambuliaji wake, Sergio Aguero katika pambano hilo baada ya juzi kamera kumwonyesha akimtwanga kiwiko cha koo mlinzi mahiri wa West Ham, Winston Reid katika pambano baina ya timu zao.

City iliichapa West Ham mabao 3-1 katika Uwnaja wa Etihad, lakini kasheshe kubwa ilitokea katika dakika ya 76 ya pambano hilo wakati Aguero alipoonekana akimtwanga kiwiko cha koo Reid ambaye hakuweza kuendelea na pambano hilo na nafasi yake ikachukuliwa na Jonathan Calleri.

Mwamuzi wa pambano hilo, Andre Marinner hakuliona tukio hilo lakini kama akijiridhisha baadaye kuwa angeona angeweza kumwonyesha kadi nyekundu Aguero,  basi FA ya England itamfungulia mashtaka staa huyo na atafungiwa mechi tatu kama akipatikana na hatia.

Baada ya wikiendi ijayo ya mechi za kimataifa, City na United zitakumbana katika dimba la Trafford mnamo Septemba 10 na kama Aguero akichukuliwa hatua za kinidhamu na kufungiwa basi atalikosa pambano hilo muhimu linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani kote. Kocha wa Man City, Pep Guardiola alidai hakuliona tukio hilo la Aguero kumpiga kiwiko Reid huku akisema anasubiri kuona picha za marudio kujua kama ni kweli nyota wake huyo wa kimataifa wa Argentina alifanya hivyo.

“Sikuona chochote. Tutaona unachokisema katika Televisheni na baada ya hapo tutaona kitakachotokea. Mimi ni mgeni hapa kwa hiyo sijui wanafanyaje kazi. Sikuona chochote kwa hiyo sina cha kuongea. Nina matumaini hakuna kitakachotokea. Kama ikitokea tutakubali na kufanyia kazi. Kama tutampoteza basi itakuwa tumempoteza tu. Bado tutacheza 11 katika mechi dhidi ya Manchester United,” alisema Guardiola.

Hata hivyo, Kocha wa West Ham, Slaven Billic alidai hakumtoa Reid kwa sababu ya kuumia, badala yake alifanya hivyo kwa ajili ya mbinu za mchezo huku akitaka kuongeza mshambuliaji mmoja na kumtoa mlinzi kwa sababu timu yake ilikuwa nyuma kwa bao moja.

“Hapana, sikuona kabisa. Tulikuwa tunajaribu kufanya mabadiliko na sikuona kabisa na ndiyo maana sikukasirishwa. Nilikasirishwa kidogo kwa sababu nilikuwa nataka kufanya mabadiliko na Winston alikuwa nje huku Calleri akiwa bado hajaingia ndani. Hayo ndiyo yalikuwa mazungumzo yangu na mwamuzi wa akiba.

Naye kiungo wa West Ham, Mark Noble aliripotiwa akiwaambia waandishi wa habari kwamba hakuona tukio hilo lakini anafahamu kuwa Reid hakuweza kuongea baada ya kumalizika kwa pambano hilo akilalamika kuumia katika koo.

“Sikuona. Sikuona kilikuwa ni kitu gani lakini ukweli ni kwamba hawezi kuongea kwa sasa. Anasema kuna kitu kilimpiga katika koo,” alisema Noble mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo juzi.

Pambano la Manchester United na Manchester City linasubiriwa kwa hamu na mashabiki duniani kote likiwa ni pambano la kwanza baina yao msimu huu huku kila timu ikiwa imeshinda mechi zake tatu za kwanza na kufikisha pointi tisa.

Pia litakuwa pambano la kwanza baina ya makocha Pep Guardiola na Jose Mourinho ambao wamekuwa katika upinzani mkubwa tangu wakiwa Hispania.