Guardiola kuwapiga chini mastaa 11

Pep Guardiola

MANCHESTER, ENGLAND

KOCHA Mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola amekiri kwamba atapitisha fagio la kutibua wachezaji wengi sana kwenye kikosi hicho mwisho mwa msimu huu.

Imeelezwa kwamba kuna wachezaji 11 ambao waliisaidia Man City kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu England, Kombe la FA na mataji mawili ya Kombe la Ligi katika kipindi cha miaka minane na nusu tangu Sheikh Mansour alipoichukua timu hiyo, watapigwa chini mwisho wa msimu huu.

Pablo Zabaleta, Gael Clichy, Bacary Sagna, Jesus Navas na Willy Caballero hawa mikataba yao itakuwa imefika mwisho.

Wachezaji wengine, Joe Hart, Samir Nasri, Eliaquim Mangala na Wilfried Bony waliotolewa kwa mkopo hawahitajiki tena warudi kwenye kikosi hicho pindi mikopo yao itakapofika tamati mwisho wa msimu.

Kuna wasiwasi mkubwa pia kuhusu hatima ya beki Vincent Kompany, ambaye kwa siku za karibuni amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha na mchezaji mwingine aliye kwenye mashaka makubwa ni Aleksandar Kolarov.

Guardiola alisema: “Ni suala la miaka mitano ijayo au 10 hivi. Ndiyo, suala la kubadili timu ni kawaida. Kocha amebadilika na wachezaji ni lazima wabadilike pia.”