Guardiola kuchenji gia angani

Monday January 9 2017

 

Manchester, England. PEP Guardiola amekiri kwamba hawezi tena kubadili soka la England na anachopaswa kukifanya ni yeye kubadili staili yake ya uchezaji.

Kocha huyo wa Manchester City amekiri kwamba, amekuwa akifanya makosa msimu huu kutokana na kung’ang’ania staili ya uchezaji akiamini England nzima itabadilika, lakini kwa sasa ni yeye ndiye anayepaswa kubadilika ili kuendana na soka la nchi hiyo.

Guardiola aliwanunua kipa mwenye uwezo wa kuuchezea mpira Claudio Bravo pamoja na beki mchezeshaji John Stones baada ya kutua Man City, lakini imegundua kuwa soka la England halihitaji kabisa mambo hayo na lenyewe lipo tofauti kabisa.

Wachezaji hao na mfumo wake amejikuta ukimgharimu kutokana na kikosi chake kuambulia vichapo kwenye Ligi Kuu England na hivyo, kuwa timu iliyofungwa mara nyingi zaidi kuliko yeyote kati ya zilizopo kwenye Sita Bora ya msimamo wa ligi hiyo kwa msimu huu.

“Siwezi kubadili soka la England na sitaki tena kufanya hivyo. Kilichopo ni mimi kubadilika. Ndiyo maana nipo hapa kubadilika.

“Ni hivyo. Sitaki maisha yangu yote ya soka nifanye kitu kimoja kwa miaka 15 au 20 kama kocha, inaboa.

“Kama ni hivyo, basi ningeendelea kubaki Barcelona, nyumbani kwangu,” alisema Guardiola.