Fifa kumlipa Khedira Pauni 20,548 kwa siku

Tuesday November 19 2013

 

MUDA halisi unaohisiwa atakuwa nje ya uwanja ni miezi sita, lakini itategemea maendeleo yake baada ya kufanyiwa upasuaji na watakachosema madaktari wa Real Madrid.

Lakini, ukubwa wa tatizo linalomkabili imeelezwa kwamba itakuwa maajabu kumwona kiungo Mjerumani Sami Khedira akirudi tena uwanjani msimu huu baada ya kuumia goti katika mechi ya kirafiki dhidi ya Italia iliyofanyika Ijumaa iliyopita.

Na kwa kipindi chote hicho Real Madrid itacheza bila ya huduma ya mchezaji wao huyo, aliyeumia akiitumikia Ujerumani kwenye mechi za kirafiki za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lakini klabu hiyo italipwa fidia ya pesa. Kuanzia siku 29 ya mchezaji huyo kukaa nje, Fifa itawajibika kulipa Pauni 20,548 kwa siku atakayokuwa nje mchezaji husika ikiwa ni sehemu ya fidia kutokana na kuiingizia gharama klabu kwa mchezaji huyo kuumia kwenye mechi za kimataifa.

Kwa utaratibu huo, Real Madrid itaanza kupokea pesa za Fifa kuanzia Desemba 14 mwaka huu na hilo litaendelea hadi hapo madaktari watakapothibitisha kwamba mchezaji huyo yupo fiti kwa ajili ya kurejea uwanjani.

Mwaka jana Real Madrid ilipokea jumla ya Pauni 1.1 Milioni kutokana na majeruhi ya Mbrazili Marcelo aliyeumia akiitumikia Brazil.