Fellaini apigwa misumari

Kiungo wa Manchester United, Marouane Fellaini

Muktasari:

Fellaini aliingia uwanjani katika dakika za majeruhi akichukua nafasi ya kiungo mshambuliaji, Henrikh Mkhitaryan kwa ajili ya kwenda kusaidia kulinda uongozi wa bao 1-0 wa Manchester United iliyokuwa inaelekea kuchukua pointi tatu muhimu.

NI Marouane Fellaini kila kona. Sio kwa mema, bali kwa mabaya. Ni kama vile kila mtu amemgeuka baada ya kosa la kijinga alilofanya juzi usiku katika pambano kati ya Manchester United dhidi ya Everton na kusababisha penalti.

Fellaini aliingia uwanjani katika dakika za majeruhi akichukua nafasi ya kiungo mshambuliaji, Henrikh Mkhitaryan kwa ajili ya kwenda kusaidia kulinda uongozi wa bao 1-0 wa Manchester United iliyokuwa inaelekea kuchukua pointi tatu muhimu.

Hata hivyo, badala yake alimchezea rafu katika eneo lake la hatari kiungo wa kimataifa wa Senegal, Idrissa Gueye dakika chache tu baada ya kuingia na hivyo mwamuzi kutoa penalti ambayo ilifungwa na mlinzi wa kushoto, Leighton Baines.

Na sasa Fellaini amegeuka kuwa habari ya mjini na kichekesho kikubwa huku akishambuliwa kila kona na mashabiki wa Man United pamoja na wachambuzi wa soka wakiongozwa na mlinzi wa zamani wa Manchester United, Gary Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka.

“Ni takataka tu kutoka kwa Fellaini. Ni wazi kwamba unapofanya faulo ndani ya boksi basi unakuwa katika hatari ya kutoa penalti. Ni upuuzi tu kutoka kwake. Hii haina uhusiano na kocha. Kocha alifanya mabadiliko kwa sababu sahihi na mchezaji alimwangusha,” alisema Neville.

“Ni aibu sana kwa mchezaji mwenye uzoefu. Alikuja kwa ajili ya kumaliza mchezo. Hakuwa na utulivu na ilionekana wazi kwamba tatizo hilo lilikuwa linakuja. Aliingizwa uwanjani kwa ajili ya kushughulika na mipira mirefu iliyokuwa inaingia katika boksi. Unaweza kuona kulikuwa na maana kuingizwa kwake lakini akafanya jambo la kijinga,” aliongeza Neville.

“Ulikuwa ujinga kutoka kwa mchezaji wa kimataifa. Huwezi kulilaumu benchi la ufundi. Alifanya ujinga tu,” aliongeza Neville.

Naye staa wa zamani wa England, Gary Lineker ambaye kwa sasa ni mchambuzi maarufu wa soka aliikejeli rafu ya Fellaini ambaye ni kiungo wa zamani wa Everton akidai “Kiwango bora zaidi ambacho Fellaini ameonyesha tangu achezee Everton.”

Naye kiungo wa zamani wa Everton, Lee Osman ambaye alicheza na Fellaini katika klabu ya Everton amedai kwamba hakushangazwa na rafu hiyo ya Fellaini kwa Gueye kwa sababu hizo ni tabia zake tangu wakiwa mazoezini Everton.

“Alikuwa kama hivyo wakati tupo naye. Alikuwa hivyo hivyo hata mazoezini ukija mbele yake lazima akuzuie kwa miguu yake au akukwatue. Tulipokuwa tunacheza naye tulikuwa tunamtaka akae mbali na boksi. Alikuwa mzuri zaidi katika eneo la adui,” alisema Osman.

Hata hivyo, kocha wa United, Jose Mourinho amejitetea kwa kitendo chake cha kumuingiza Fellaini baada ya kuanza kupokea lawama kwa mashabiki mbalimbali wa United ambao wanamlaumu kwa kumuingiza staa huyo.

“Nadhani inabidi mfahamu soka kuliko mnavyolifahamu sasa. Everton sio timu ya pasi nyingi tena kama ilivyokuwa zamani. Wanacheza mipira mirefu. Kipa wao anacheza hivyo, Ashley Williams yuko hivyo, Ramiro Funes Mori yuko hivyo. Kila mtu yuko hivyo. Unapokua na mchezaji mwenye urefu zaidi katika benchi unamuingiza acheze mbele ya walinzi wa kati kwa ajili ya kuisaidia timu kushinda mechi,” alisema Mourinho.

United ambayo ilikuwa inatafuta ushindi wake wa tatu wa Ligi ndani ya mechi 11 ilipata bao la kuongoza kupitia kwa staa wake wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic aliyemalizia mpira mrefu na kuubetua juu ya kipa, Martin Stekelenburg aliyetoka ovyo langoni mwake.