El Hadary kibabu cha Afcon 2017

Saturday January 7 2017

KIPA veterani, Essam El Hadary amejumuishwa kwenye kikosi cha mwisho cha Misri kitakachokwenda kwenye fainali za Afcon 2017 zitakazoanza Januari 14 hadi Februari 5, mwaka huu, huko Gabon na sasa anasubiri kuandika rekodi mpya.

El Hadary ametimiza umri wa miaka 43 na kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye historia ya michuano hiyo ya Afrika, akiizidi rekodi iliyowekwa na Hossam Hossan mwaka 2006 aliyekuwa akiichezea pia Misri.

Kocha Hector Cuper mwezi uliopita aliwashangaza wengi baada ya kumtema fowadi wa Zamalek, Bassem Morsi, ambaye alikuwa akianza katika kikosi cha kwanza cha nchi hiyo kilichocheza mechi mbili za karibuni za kufuzu Kombe la Dunia Oktoba na Novemba mwaka jana.

Ni wachezaji wanne tu ndiyo waliobakizwa kwenye kikosi hicho kutoka wale waliokuwapo mara ya mwisho Misri iliposhiriki michuano hiyo na kushinda ubingwa mwaka 2010. Mastaa hao ni El Hadary, Ahmed Elmohamady, Mohamed Abdelshafi na Ahmed Fathi.

Misri, ambayo imekosa michuano mitatu iliyopita ya ubingwa huo wa Afrika, imepangwa kwenye Kundi D na itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Mali, Januari 17.