Conte atema ubingwa

Tuesday February 14 2017

ASIKWAMBIE mtu hakuna kitu kigumu kama kuongoza ligi na kisha timu zilizopo nyuma yako zote kali, lazima presha ipande.

Antonio Conte na kikosi chake cha Chelsea anaongoza Ligi Kuu England tena kwa tofauti ya pointi 10, lakini amechungulia timu zinazomfukuzia, akasema timu zote ndani ya Top Six yoyote inaweza kuwa bingwa.

Conte amepata wasiwasi huo baada ya kushindwa kuongeza pengo la pointi kufuatia sare ya bao 1-1 ugenini kwa Burnley.

Chelsea walikumbana na wakati mgumu uwanjani Turf Moor juzi Jumapili, lakini Burnely inaelezwa kuwa ni timu ya tatu kuwa na rekodi nzuri inapokuwa nyumbani nyuma ya Chelsea na Tottenham.

“Kuna mechi 13 kabla ya ligi kumalizika,” alisema Conte, ambapo pengo la pointi linaweza kupungua na kuwa pointi nane kama Manchester City watakuwa wameshinda mechi yao dhidi ya Bournemouth usiku wa jana Jumatatu.

“Kuna watu wanadhani ligi imekwisha, mimi nawaambia, hapana. Kuna timu sita ambao naamini yoyote inaweza kuwa bingwa na chochote kinaweza kutokea.”

Timu zilizopo kwenye Top Six ni Tottenham, Arsenal, Liverpool, Man City na Manchester United na timu hizo kuanzia ya pili hadi ya sita zimetofautiana pointi mbili tu, zitaongezeka kuwa tatu kama Man City itakuwa imeshinda mechi yake.