Chelsea dakika 512 bila kuruhusu bao

Muktasari:

Juzi ilikuwa ugenini Riverside ikikipiga na Middlesbrough na kushinda bao 1-0 inamaanisha kwamba Chelsea sasa imecheza dakika 512 bila ya kuruhusu nyavu za lango lake kuguswa.

WALE watoto wa darajani pale London walianza ligi kama mzaha, lakini kadiri dakika zinavyoyoyoma inaonekana wazi kwamba hawatanii. Ndiyo, Chelsea sasa inaonekana kuanza kuvunjavunja rekodi za kibishi katika Ligi Kuu ya England.

Juzi ilikuwa ugenini Riverside ikikipiga na Middlesbrough na kushinda bao 1-0 inamaanisha kwamba Chelsea sasa imecheza dakika 512 bila ya kuruhusu nyavu za lango lake kuguswa.

Mara ya mwisho kuruhusu bao ilikuwa ni katika kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Arsenal Septemba 24 mwaka huu.

Mara ya mwisho kucheza muda mrefu bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa ilikuwa miaka 10 iliyopita wakati langoni akiwa kipa, Petr Cech ambaye kwa sasa yupo Arsenal, huku katika benchi akiwa Kocha, Jose Mourninho ambaye kwa sasa yupo Manchester United.

Kwa kucheza dakika hizo bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa hii ina maana kuwa kipa wao wa kimataifa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois amecheza saa tisa na dakika 10 bila ya kufungwa katika Ligi Kuu ya England.

Mara baada ya kufungwa na Arsenal, Kocha Muitaliano wa Chelsea, Conte alibadlisha mfumo wake na kuipeleka timu katika mfumo wa 3-4-3 ambao uliifanya ishinde mechi sita na kufunga mabao 17 huku sasa ikiongoza Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi 28 ikifuatiwa na Liverpool na Manchester City zenye pointi 27.

Conte anaonekana kunogewa na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza cha sasa ambapo hajabadilisha kikosi hicho katika mechi tano mfululizo kuanzia pambano dhidi ya Hull City Oktoba Mosi mpaka juzi.

Kocha Conte anaonekana kupata kombinesheni nzuri ya mabeki wake wa kati, David Luiz, Gary Cahill na Cesar Azpilicueta huku Mnigeria, Victor Moses akicheza kama beki wa kupanda na kushuka upande wa kulia, Marcos Alonso akicheza kama beki wa kupanda wa kushuka upande wa kushoto.

Viungo wawili wa kati ni N’Golo Kante na Nemanja Matic ambao baada ya kusuasua katika pambano dhidi ya Arsenal wameonekana kuimarika zaidi na mbele yao wanacheza Pedro na Eden Hazard huku Diego Costa akisimama mbele.

Baada ya kusuasua msimu uliopita, mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania mzaliwa wa Brazil, Diego Costa anaonekana kurudi katika fomu yake kwa mara nyingine tena huku juzi akifunga bao la ushindi katika pambano hilo dhidi ya Middlesbrough.

Costa amefunga mabao saba katika mechi saba za mwisho za ugenini huku pia akiwa mchezaji wa Ligi Kuu ambaye amehusika katika mabao mengi kuliko mchezaji mwingine yeyote katika ligi hiyo. Amehusika katika mabao 13 akifunga mabao 10.

Mchezaji ambaye anaonekana kuathirika na kiwango cha juu cha Chelsea kwa sasa ni nahodha, John Terry ambaye licha ya kuwa fiti lakini amekuwa akisugua benchi katika nafasi za mabeki watatu wakali, David Luiz, Gary Cahill na Cesar Azpilicueta ambao wanaonekana kuelewana kwa sasa.

Kuibuka kwa Moses pia kumewashangaza wengi baada ya winga huyo wa kimataifa wa Nigeria kutabiriwa kwamba huenda siku zake za kukipiga Stamford Bridge zilikuwa zimefikia ukingoni baada ya kuondolewa sana kwa mikopo katika zama za makocha waliopita.

Mambo yamekuwa magumu kwa Mnigeria mwenzake, Obi Mikel ambaye hajacheza hata dakika moja chini ya utawala wa Conte na kuna uwezekano mkubwa akaondoka Chelsea katika dirisha la Januari.