Bolasie benchi mwaka mzima

Saturday January 7 2017

WINGA matata wa Everton na DR Congo huenda akawa nje ya uwanja kwa mwaka mzima kutokana na kukabiliwa na maumivu makali ya goti.

Kocha Mkuu wa Everton, Ronald Koeman alisema fowadi huyo amepata majeraha ambayo yatamfanya awe nje ya uwanja kwa muda usiopungua mwaka mmoja.

Bolasie (27), alipata majeruhi hayo ya goti lake la kulia katika mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Manchester United kwenye Ligi Kuu England iliyofanyika Desemba 4 mwaka jana.

Kocha wa Everton, Koeman alisema Jumatano iliyopita:

“Itakuwa kama miezi 11 hadi 12 kabla hajarejea uwanjani. Ni pigo kubwa, lakini atarejea tu.”

Bolasie atafanyiwa upasuaji wa pili wiki chache zijazo ili kurekebisha tatizo linalomsababishia maumivu hayo.

Staa huyo wa kimataifa wa DR Congo amenaswa na Everton akitokea Crystal Palace kwa ada ya Pauni 25 milioni na amekuwa akicheza kila mechi ya Ligi Kuu Engla msimu msimu huu hadi alipoumia.

Katika kuziba pengo la Bolasie, Everton inaweza kumnasa winga wa Kidachi, Memphis Depay kutoka Man United, ambaye kwa sasa anasugua tu benchi na tayari ameruhusiwa kuondoka Old Trafford.