Bei zao sokoni ujipange

Muktasari:

Lakini, ndiyo hivyo, soko la wanasoka liko juu, hasa ukingatia mwanasoka mwenyewe awe Griezmann au Mbappe. Dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi linatarajia kushuhudia pesa ndefu zikimininika hata kutokana na idadi ya wachezaji wanaowindwa wote kuwa wenye thamani kubwa.

MANCHESTER United imeripotiwa kuweka mezani Pauni 95 milioni kumnasa kinda wa AS Monaco, Kylian Mbappe. Papo hapo, wameripotiwa kumnasa supastaa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann kwa Pauni 86 milioni. Ni hesabu za pesa ndefundefu tu.

Lakini, ndiyo hivyo, soko la wanasoka liko juu, hasa ukingatia mwanasoka mwenyewe awe Griezmann au Mbappe. Dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi linatarajia kushuhudia pesa ndefu zikimininika hata kutokana na idadi ya wachezaji wanaowindwa wote kuwa wenye thamani kubwa.

Tazama orodha hii ya mastaa 10 wanaowindwa; Griezmann, Mbappe, Sergio Aguero, Alexis Sanchez, Mesut Ozil, Neymar, Robert Lewandowski, Willian, Eden Hazard na David De Gea. Nani mwenye unafuu wa bei hapo? Wote hao, ukihitaji saini zao tu, lazima ikutoke pesa ndefu. Wanauzwa bei ghali sana.

Griezmann, anayetajwatajwa mara nyingi kwamba, ataenda Old Trafford mwisho wa msimu, bei yake sokoni inatajwa kuwa Euro 80 milioni, thamani ambayo imeongezeka kwa kasi tangu mwaka 2014, ambapo alidaiwa bei yake sokoni kuwa Euro 30 milioni. Supastaa wa Barcelona, Neymar, anayetajwa kuwa kwenye dili la kujiunga na moja ya timu za Ligi Kuu England, ametajwa kuwa na thamani ya Euro 100 milioni sokoni hadi kufikia Februari mwaka huu. Wakati anatua Barcelona mwaka 2013, Neymar alidaiwa kuwa na thamani ya Euro 50 milioni, hivyo soko lake limepanda kwa asilimia 100.

Hazard, ambaye jina lake halikauki kwenye midomo ya mabosi wa Real Madrid kutokana na kuisaka huduma yake ana thamani ya Pauni 59.5 milioni. Winga huyo wa Kibelgiji mgumu kukabika uwanjani wakati anatua Chelsea mwaka 2012, thamani yake ilikuwa Pauni 34 milioni. Staa mwingine dirisha la usajili likifunguliwa tu, huwezi kumwona akiendelea kubaki kwenye klabu yake ya sasa ni Alexis Sanchez. Supastaa huyo wa Chile, thamani yake wakati anatua Arsenal ilikuwa 32.4 milioni mwaka 2014, lakini hadi kufikia mwaka huu, bei yake sokoni imeongezeka na kufikia Pauni 55.25 milioni, huku nyota mwenzake wa Emirates, Ozil akibaki na thamani yake ile ile ya Pauni 50 milioni kama alivyotua Arsenal mwaka 2014. Mwaka 2015, Ozil thamani yake sokoni ilishuka hadi Pauni 40 milioni kabla ya kuipandisha kwa Pauni 10 milioni hadi kufikia mwaka huu. Sergio Aguero asiyejielewa hatima yake klabuni Manchester City thamani yake sokoni kwa sasa ni Pauni 63 milioni huku Willian wa Chelsea thamani yake sokoni ikiwani Euro 32 milioni. Mwaka 2013, Mbrazili huyo bei yake sokoni ilikuwa Euro 35 milioni, hivyo ameshuka. Straika anayezitoa udenda klabu nyingi za Ulaya, Robert Lewandowski, anayekipiga huko Bayern Munich, bei yake sokoni ni Pauni 68 milioni. Makali ya Lewandowski yamepandisha thamani yake sokoni kwani, mwaka 2014 bei yake ilikuwa Pauni 42.5 milioni. Kipa David De Gea anajiandaa kuweka rekodi ya kuwa kipa ghali duniani baada ya thamani yake sokoni kwa sasa kuwa Euro 40 milioni. Real Madrid wanamtaka kipa huyo Mhispaniola, ambaye miaka sita iliyopita, thamani yake sokoni ilikuwa Euro 18 milioni.

Ukiitafuta bei yake sokoni kwa sasa, kinda Mbappe ni Euro 10 milioni tu. Katika kuwashawishi AS Monaco, Man United imeamua kuipandisha thamani ya soko ya kinda huyo anayefananishwa na Thierry Henry hadi kufikia Pauni 95 milioni, ambazo zinadaiwa wababe hao wa Old Trafford wameweka mezani.