BIFU TENA: Mourinho amuweka kando Ronaldo

Muktasari:

WANATOKA taifa moja lakini hawajawahi kupendana wala kupikika chungu kimoja. Ni Jose Mourinho na Cristiano Ronaldo. Wote ni mastaa katika kazi zao na wanapendwa dunia nzima, lakini hawajawahi kupendana hata siku moja.

WANATOKA taifa moja lakini hawajawahi kupendana wala kupikika chungu kimoja. Ni Jose Mourinho na Cristiano Ronaldo. Wote ni mastaa katika kazi zao na wanapendwa dunia nzima, lakini hawajawahi kupendana hata siku moja.

Mourinho amepigilia msumari wa mwisho kwa Ronaldo baada ya kutaja wachezaji wake bora wa muda wote duniani, lakini akamuweka kando na kuamua kumuweka hasimu wa Ronaldo katika orodha hiyo, Lionel Messi.

Achilia mbali Messi, katika orodha hiyo Mourinho amewaweka mastaa wakongwe, Pele wa Brazil na Diego Maradona wa Argentina ambao wamewaingiza mashabiki katika vita ya muda mrefu kuhusu nani ni bora zaidi kati yao. Alipoulizwa ataje wachezaji wake bora watatu wa muda wote, Mourinho alijibu “Kwangu wachezaji watatu bora katika historia ni Messi, Pele na Maradona.”

Baadaye, mtoto wa kocha huyo, Jose Jr ambaye anakipiga katika timu ya vijana ya Fulham kama golikipa alirudia kutuma maoni ya Baba kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii akisisitiza kile ambacho alikiongea baba yake.

Mourinho alifanya kazi na Ronaldo kwa miaka mitatu Real Madrid kati ya mwaka 2010 hadi 2013 na katika msimu wake wa mwisho mchezaji huyo alitwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mbele ya Messi. Hata hivyo wakati huo, Mourinho alionekana kumpaisha zaidi Ronaldo labda kwa sababu alikuwa anamsaidia kazi yake.

“Ni mchezaji bora. Mchezaji bora zaidi duniani. Pengine ni mchezaji bora kuwahi kutokea. Nilimuona Maradona mara kadhaa. Sikuwahi kumuona Pele, lakini Ronaldo anatisha. Huyu mtu ni bora.” Alisema Mourinho mwaka 2013.

Ronaldo, ambaye ana umri wa miaka 31 kwa sasa alichaguliwa tena kuwa mwanasoka wa dunia mwaka 2014 lakini akashindwa na Messi mwaka 2015. Na sasa kauli ya Mourinho inalenga zaidi katika kudharau mafanikio ya Ronaldo ya kutwaa michuano ya Euro 2016.Wakati Ronaldo akifanya hilo, Messi alichemka kwa mara ya pili mfululizo kutwaa michuano ya Copa Amerika akiwa na kikosi cha Argentina baada ya kuchapwa kwa matuta na Chile katika fainali nchini Marekani.

Bifu la Ronaldo ni la muda mrefu na lilianzia wakati Mourinho akiwa na Chelsea katika awamu yake ya kwanza huku Ronaldo akiwa na Manchester United ambao Ronaldo aliwahi kumkebehi Mourinho kwa kupenda kulalamika mambo mengi kuhusu Manchester United.Baadaye Mourinho alitoa kauli za dharau kwa Ronaldo akidai kwamba nyota huyo, ambaye nyakati hizo alikuwa kinda, alikuwa ameathirika na ukosefu wa elimu sahihi pamoja na janga la kukulia katika umaskini.

Bifu hilo liliendelea hata walipokutana Santiago Bernabeu ambapo kwa mujibu wa kitabu cha maisha ya Ronaldo kilichoandikwa na mwandishi mahiri wa Hispania, Guillem Balague anadai kwamba Ronaldo alimshutumu Mourinho kwa kutengeneza hali mbaya ya hewa klabuni hapo.

Balague anaandika kuwa hali ilikuwa mbaya wakati Fulani ambapo Ronaldo aliwahi kubwatukiana na Mourinho wakati wa mapumzio wa pambano moja la La Liga akikerwa na tabia ya kocha huyo kupenda wachezaji wajihami muda mwingi.

“Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba Cristiano ilibidi ashikwe (Wengine wanasema alishikwa na Casillas, wengine Arberloa, wengine, Khedira, wengine Sergio Ramos) kwa ajili ya kuzuia wasipigane. Ronaldo aliona kauli za Mourinho hazikuwa za kisoka zaidi ya kumshambulia yeye binafsi. Uhusiano wa Mourinho na Ronaldo haukuweza kuwa poa tena.”