Ancelotti amteua mwanaye ukocha Bayern

Muktasari:

  • Davide Ancelotti atakuwa na kazi ya kumsaidia baba yake kuiongoza timu hiyo ya Ujerumani kuhakikisha inafanya vizuri kwenye Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kuweka rekodi ya kuwa baba na mwanaye kuwa makocha wa timu moja katika historia ya Ligi Kuu ya nchi hiyo

Munich,Ujerumani. FAMILIA vipi? Carlo Ancelotti amemteua mwanaye kuwa kocha msaidizi katika kikosi cha Bayern Munich.

Davide Ancelotti atakuwa na kazi ya kumsaidia baba yake kuiongoza timu hiyo ya Ujerumani kuhakikisha inafanya vizuri kwenye Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kuweka rekodi ya kuwa baba na mwanaye kuwa makocha wa timu moja katika historia ya Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Davide mwenye umri wa miaka 27 alishindwa kufanya mambo ya maana akiwa mchezaji wakati alipokuwa kwenye timu ya vijana ya AC Milan. Baadaye alikwenda kusoma Sayansi ya Michezo kabla ya kubamba dili la ukocha wa viungo klabuni Real Madrid, huku baba yake akiwa kocha wa timu hiyo.

“Nitasaidiana na makocha wengine mazoezini na kwenye maandalizi kabla ya mechi. Nitakuwa kwenye uwanja wa mazoezi kujaribu kuyarahishisha na kuzungumza kwa lugha nyepesi ili ifahamike zaidi,” alisema Davide.

Bayern Munich itaanza msimu wake mpya wa Bundesliga kesho Ijumaa kwa kumenyana na Werder Bremen uwanjani Allianz Arena.