AMEVURUGWA: Kipigo cha Pep Guardiola ni rekodi

PEP  GUARDIOLA : Amenasa jumla ya vikombe sita vya Ligi Kuu akiwa na timu za Barca  na Bayern Munich

Muktasari:

Kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton juzi mchana ni kipigo cha kwanza kikubwa zaidi kwa Guardiola katika mechi za ligi baada ya kufundisha soka katika nchi za Hispania na Ujerumani huku akitamba na Barcelona na Bayern Munich.

LiverPool,England. AMEVURUGWA. Pep Guardiola amevurugwa kabisa na Ligi Kuu England. Ni katika ligi hii ndipo anaonekana amechanganyikiwa na haelewi anachofanya. Sasa amepokea kipigo chake kikubwa zaidi katika ligi tangu aanze kufundisha soka.

Kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton juzi mchana ni kipigo cha kwanza kikubwa zaidi kwa Guardiola katika mechi za ligi baada ya kufundisha soka katika nchi za Hispania na Ujerumani huku akitamba na Barcelona na Bayern Munich.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Guardiola kupigwa mabao 4-0 akiwa kocha. Tayari akiwa na Bayern Munich alichapwa mabao 4-0 na Real Madrid lakini ilikuwa ni katika pambano la ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Akiwa na City hii pia alichapwa mabao 4-0 na Barcelona likiwa ni pambano jingine la ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton juzi kilikuwa kibaya zaidi katika mechi zake 275 za ligi alizosimamia katika nchi za Hispania, Ujerumani na sasa hivi England ambako maisha yake ya ukocha yameanza kupata wakati mgumu.

Kwa kichapo cha juzi, City inakuwa imefungwa mechi nne katika nane zilizopita na pengo kati yao na Chelsea kwa sasa ni pointi 10. Tayari Guardiola amenyanyua mikono juu na kukiri kwamba hawana nafasi ya kushika nafasi ya kwanza na kuchukua taji.

“Nafasi ya kwanza, ndio, nafasi ya kwanza kuna pengo la pointi 10 na hizo ni nyingi sana. Nafasi ya pili kuna pengo la pointi tatu kwa hiyo ebu tuone. Itakuwa kosa kubwa kumlaumu mtu mmoja, lakini ni kweli kwamba hii ni mara yangu ya kwanza kufungwa mabao mengi hivi,” alisema Guardiola.

“Haijawahi kunitokea huko nyuma. Ndiyo maana inabidi nijue sababu ni nini. Niliongea na wachezaji wiki tatu zilizopita wasahau msimamo wa ligi na kujikita katika mechi inayofuata. Nataka tuwe bora zaidi na zaidi na tujisikie tunaweza kufunga mabao. Tukifanya hivyo hatutapata matatizo nyuma. Washambuliaji wetu watajiamini zaidi.”

Katika pambano hilo lililopigwa uwanjani Goodson Park, Guardiola aliadhiriwa zaidi na makinda wawili, Tom Davies na Ademola Lookman ambao wote walifunga mabao yao ya kwanza katika Ligi Kuu ya England.

Wakati Davies akiwa amekulia katika shule ya soka ya Everton, Ademola amenunuliwa na Everton katika dirisha hili la majira ya baridi akitokea Charlton Athletic kwa dau la Pauni 10 milioni na hivyo kuanza vyema katika Ligi Kuu ya England.

Mabao mengine katika pambano hilo yalifungwa na nyota wawili wa kimataifa wa Ubelgiji, Romelu Lukaku na Kevin Mirallas ambaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Lookman katika dakika za mwisho za pambano hilo.

Mtihani mwingine unamkabili Guardiola Jumamosi katika pambano jingine gumu la nyumbani dhidi ya Tottenham ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 sawa na Liverpool lakini ina tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya hapo, Guardiola ambaye kikosi chake kinashika nafasi ya tano atakwenda ugenini kukipiga na West Ham ambayo imeanza kurudisha makali yake ya msimu uliopita baada ya kuanza ovyo msimu huu ikiwa imehamia katika uwanja wake mpya wa London Stadium.

Kumekuwa na mashaka makubwa na juu ya uwezo wa Guardiola kukabiliana na soka la nguvu la Ligi Kuu England huku ushindani ukiwa mkubwa tofauti na Hispania na Ujerumani.