WENGER NOMA: Aamua kuvunja benki katika usajili

Staa wa Deportivo La Coruna, Lucas Perez

Muktasari:

  • Mfaransa huyo amefanikiwa kutoa dau la Pauni 17 milioni kumnasa staa wa Deportivo La Coruna, Lucas Perez ambaye ataimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambaye mpaka jana jioni alikuwa amefaulu vipimo vya afya. Pia Wenger amekubaliwa katika dau lake la Pauni 35 milioni kumnasa mlinzi mahiri wa kimataifa wa Ujerumani, Shokrodon Mustafi.

LONDON, ENGLAND

LABDA wahenga walikuwa sahihi waliposema mcheka mwisho ndiye hucheka sana. Huenda sasa mashabiki wa Arsenal wakashusha pumzi kwa nguvu baada ya Kocha wao, Arsene Wenger kukunjua makucha yake na kutumia pesa alizobana kwa muda mrefu.

Wenger anayesifika kwa ubahili alikuwa akilalamikiwa na mashabiki wa Arsenal, wachezaji wa zamani wa timu hiyo pamoja na wachambuzi wa soka kwa kushindwa kushindana katika dirisha la uhamisho na kumnunua mchezaji mmoja tu katika dirisha hili.

Mfaransa huyo amefanikiwa kutoa dau la Pauni 17 milioni kumnasa staa wa Deportivo La Coruna, Lucas Perez ambaye ataimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambaye mpaka jana jioni alikuwa amefaulu vipimo vya afya. Pia Wenger amekubaliwa katika dau lake la Pauni 35 milioni kumnasa mlinzi mahiri wa kimataifa wa Ujerumani, Shokrodon Mustafi.

Kwa jumla usiku wa juzi, Wenger alitumia Pauni 50 kwa ajili ya mastaa hao huku akiwa na uhakika wa kumaliza shughuli nzima ya kuwasajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho Jumatano usiku na hivyo kuwashusha pumzi mashabiki wa timu hiyo.

Perez alikuwa anatakiwa na Everton huku ikidaiwa kuwa alikuwa amekwishakamilisha mazungumzo binafsi na timu hiyo, lakini Wenger aliingilia kati katika dakika za mwisho na kumshawishi staa huyo kumpatia nafasi ya kucheza Ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Msimu uliopita Perez alikuwa mmoja kati ya washambuliaji tishio katika Ligi Kuu Hispania akifunga mabao 17 katika mechi 37, ikiwemo kufunga mfululizo mabao saba katika mechi saba mfululizo kati ya Oktoba na Desemba. Pia alifunga bao katika mechi ya kwanza ya ufunguzi msimu huu dhidi ya Eibar.

Kununuliwa kwake na Arsenal kunakuja kama faraja kwa mashabiki wa Arsenal baada ya kuhofia kuwa huenda dirisha la uhamisho lingefungwa huku timu yao ikiwa na mshambuliaji mmoja tu wa kati, Olivier Giroud kutokana na majeraha ya muda mrefu ya mshambuliaji mwingine, Danny Welbeck.

Tayari katika dirisha hili, Wenger alichemsha kuwanunua washambuliaji wengine, Jamie Vardy wa Leicester, Gonzalo Higuain wa Napoli aliyehamia Juventus na Alexandre Lacazette wa Lyon aliyeamua kubaki timu hiyo.

Kwa upande wa Mustafi, mlinzi huyo anakwenda Arsenal kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo tayari imewapoteza nahodha, Per Mertesacker na Gabriel Paulista kutokana na majeraha huku Laurent Koscielny akibakia kuwa mlinzi pekee mwenye uzoefu.

Mustafi (24), anarudi tena katika soka la Kiingereza baada ya kuondoka miaka minne iliyopita. Alihamia katika klabu ya Everton akiwa na umri wa miaka 16 tu akitokea Hamburg ya kwao Ujerumani.

Hata hivyo, kutokana na uchanga wake huku Everton ikiwa na wachezaji wazoefu, alicheza mechi moja kabla ya kuuzwa kwenda Sampdoria ya Italia. Baada ya kuimarika alinaswa na Valencia na tangu hapo ameibuka kuwa mmoja kati ya walinzi mahiri wa kati barani Ulaya.

Mustafi mwenye asili ya Albania anatarajiwa kuongeza idadi ya wachezaji wa Kijerumani katika kikosi cha Arsenal ambapo ataungana na mastaa wengine wa nchi hiyo, Mertesacker, Mesut Ozil na kinda Serge Gnabry ambaye alitesa katika michuano ya Olimpiki.

Kwa manunuzi ya mastaa hao wawili, Wenger atakuwa ametumia kwa jumla kiasi cha Pauni 100 milioni kwa ajili ya matanuzi ya wachezaji wapya kikosini hapo. Awali alikuwa amefanikiwa kumnasa kiungo mahiri wa Borussia Monchengladbach, Granit Xhaka kwa dau la Pauni 35 milioni.

Mwingine ni mlinzi kinda wa Bolton Wanderers, Rob Holding aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 2 milioni tu. Holding pamoja na Calum Chambers walichemsha katika pambano la kwanza dhidi ya Liverpool.