Kiwango:Van Gaal atofautiana na Ferguson

Muktasari:

Mdachi huyo amewataka wachezaji wake kushinda mechi zao huku wakicheza soka la kiwango cha juu ili kuwaburudisha mashabiki wanaojazana uwanjani kuitazama.

KOCHA Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal amefichua kwamba hapendi kuiona timu yake ikishinda huku ikicheza soka bovu uwanjani.

Mdachi huyo amewataka wachezaji wake kushinda mechi zao huku wakicheza soka la kiwango cha juu ili kuwaburudisha mashabiki wanaojazana uwanjani kuitazama.

Msimamo huo umemfanya Van Gaal atofautiane na falsafa za aliyekuwa kocha wa zamani katika klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford, Sir Alex Ferguson, ambaye alichokuwa akikitaka ni matokeo ya ushindi tu bila ya kujali timu imechezaje.

“Mimi siangalii matokeo tu,” alisema Van Gaal na kuongeza. “Hicho ndicho kikubwa nilichozungumza na Sir Alex wakati aliponiambia kwamba hakutakuwa na matatizo kama nitashinda tu. Kwangu mimi kiwango cha ndani ya uwanja ni muhimu zaidi.

“Unapocheza vizuri utashinda zaidi. Ndiyo maana nataka kuwaonyesha mashabiki na wachezaji kwamba hilo linawezekana. Kwa mfano, mechi yetu dhidi ya Hull City tulishinda 3-0 na mechi ilikuwa nzuri. Tulitawala dakika zote 90, ukweli nataka kama vile. Kwa sasa tumeweza kutawala mechi chache kwa dakika zote tisini, ninachokitaka tufanye hivyo katika kila mechi.

“Tulishinda mechi sita mfululizo na hilo limerudisha ari kwa wachezaji, lakini bado natazama kiwango hakijafikia kwenye ubora ninaoutaka.”