Woga: Wenger akiri Arsenal ilihofia kipigo

Tuesday December 23 2014kocha wa timu ya Arsenal,Arsene Wenger

kocha wa timu ya Arsenal,Arsene Wenger 

ARSENAL waoga. Kichapo cha msimu uliopita uwanjani Anfield kimebaki kumbukumbu isiyofutika kwao.

Ndiyo maana hata juzi Jumapili waliporudi tena uwanjani hapo walicheza kwa wasiwasi mkubwa wa kuhofia kichapo kama hicho.

Kocha mkuu wa kikosi hicho chenye maskani yake, Emirates, Arsene Wenger amesema kipigo cha mabao 5-1 walichokumbana nacho msimu uliopita walipokwenda kucheza uwanjani hapo kimewaathiri baadhi ya wachezaji wake na kuwapa presha kubwa juzi walipomenyana na kutoka sare ya mabao 2-2.

Kwenye mchezo huo, Liverpool ya Brendan Rodgers ilikuwa kwenye ubora mkubwa ikitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, lakini hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wakati timu hizo zilipokumbana, Liverpool ilikuwa mbele kwa mabao 4-0 hadi kufikia mapumziko.

Safari hii, straika Olivier Giroud alionekana kama anataka kuipa ushindi Arsenal uwanjani hapo Anfield baada ya kufunga bao la pili.

Lakini Martin Skrtel aligoma baada ya kufunga kwa kichwa bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi na hivyo kuwafanya Arsenal kuachwa kwa pointi nne kuifikia West Ham United iliyopo kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Baada ya mchezo huo, Wenger alisema kikosi chake kilicheza kwa woga mkubwa sana, wakikaa nyuma zaidi na kushindwa kushambulia kupata matokeo wakihofia kilichowakuta msimu uliopita.

Wenger alisema: “Tulikuwa na tatizo kwenye mtiririko wa soka letu. Hatukuwa na muda wa kutosha wa kumiliki mpira. Kwenye kipindi cha kwanza lilikuwa tatizo la kiufundi na la kisaikolojia nadhani. Pengine yale matokeo mabaya tuliyokumbana nayo hapa.

“Baadhi ya wachezaji hawakuwa kwenye ubora wao. Nadhani tulicheza kwa kusitasita sana, hasa kwenye kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili tulicheza vizuri, lakini baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-1 tulipata uoga na kurudi nyuma. Na unaposhindwa kufunga bao la tatu, upo kwenye hatari kubwa na wasiwasi na hicho ndicho kilichotokea wakatufunga bao la pili.”

Kocha Wenger hakuwa amefurahishwa na staili ya ulinzi iliyochezwa na kikosi chake katika mchezo huo hasa ikizingatiwa kwamba wapinzani walikuwa pungufu kufuatia mshambuliaji Fabio Borini kutolewa kwa kadi nyekundu.

“Nilichokiona baada ya kuwa pungufu uwanjani hatukuwa hatarini tena. Kufungwa bao la kona ni mbaya sana, lakini mbaya zaidi hakuna aliyeruka sambamba na Skrtel,” alisema Wenger.

“Sawa ni matokeo, lakini yanaumiza kwa sababu tulirudi kulinda tukiwa na mabeki wengi uwanjani na bado tukaruhusu kufungwa bao la mpira wa kutenga. Nadhani tulipaswa kulinda vizuri mipira ya kutenga.”