Neville achekelea vurugu

MANCHESTER, ENGLAND

DUNIA haitaishiwa na vita kama watu wa aina ya Gary Neville wataendelea kuzaliwa. Wakati mashabiki wa soka duniani wakihuzunishwa na vurugu zilizotokea juzi katika mechi ya Man City na Chelsea, Neville yeye ana mawazo tofauti kabisa.

Mwishoni mwa pambano hilo lililoisha kwa vurugu, City ilichapwa 3-1 na Chelsea nyumbani Etihad huku mastaa wawili wa City, Sergio Aguero Kun na Fernandinho walionyeshwa kadi nyekundu.

Aguero alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mlinzi, David Luiz, wakati Fernandinho alipewa kadi nyekundu kwa kumkaba shingo kiungo, Cesc Fabregas aliyejiingiza katika vurugu hizo ingawa alikuwa ameshatolewa uwanjani na kocha wake Antonio Conte.

Sasa, Neville, staa wa zamani wa Man United aliyegeuka mchambuzi mahiri wa soka ana mawazo tofauti akidai alizipenda vurugu hizo kwa sababu zinadhihirisha mapenzi makubwa kwa wachezaji hao na timu zao.

“Siwezi kuipenda rafu ya Aguero. Siwezi kabisa. Lakini kilichotokea mwishoni, ingawa naweza kuwa siko sahihi kusema hili lakini ukweli ni kwamba nilipenda. Watu wa Ligi Kuu hawawezi kuipenda, FA hawawezi kuipenda. Watu watafungiwa, kutakuwa na faini na mambo mengine lakini sipendi mpira ambao haujachangamka,” alianza Neville.

“Hivyo ndivyo wachezaji wanavyotetea jezi zao, wanavyowatetea wachezaji wenzao na kuonyesha mapenzi kwa jezi yako. Kunapokuwa na rafu kama ile unatazamia kuona wachezaji wenzako wakipandisha mzuka na wachezaji wengine wakijiingiza,” alisena Neville.

“Labda sipaswi kusema hivi kutokana na nafasi yangu lakini ndicho ninachofikiri na ninaweza kusema hivi tena kesho. Ndiyo, Ligi Kuu ya England ina taswira nzuri duniani kote, lakini kwa upande mwingine kila siku tunasikia jinsi wachezaji walivyokosa uzalendo na mapenzi. Sasa umeona uzalendo unavyokuwa.”

“Kila siku tunauliziwa kuhusu ugomvi wa zamani. Watu wanasema ‘Unakumbuka ule ugomvi wa Arsenal na Man United katika sehemu ya kuingilia uwanjani?’ hizo ndizo nyakati zinazoufanya mchezo wa soka uwe bora. Kuna mechi nyingi sana za kawaida siku hizi. Lakini kwa mechi kama hii nitakwenda nyumbani na kusema ilikuwa bonge la mechi. Nitaikumbuka mechi hii.”

Sasa Chelsea inaongoza ligi ikiwa na pointi 34 huku kukiwa na matarajio makubwa kwa timu hiyo kutwaa taji hilo baada ya kushinda mechi nane mfululizo huku wakifungwa mabao mawili tu katika mechi hizo.

Ingawa mambo bado na Chelsea bado itakimbizwa kwa karibu na Arsenal, Liverpool na Man City huku Man United wakinyemelea, Neville anaamini wababe hao wana nafasi kubwa ya kutwaa taji.

“Wana nafasi kubwa. Wana wachezaji ambao ni washindi katika vyumba vya kubadilishia nguo na watakuwa wanajisemea ‘Mambo mazuri’. Costa na Hazard inabidi wabakie kuwa fiti, hilo ni jambo zuri kwani wakishuka viwango ni majanga. Lakini wote wanaonekana wapo tayari. Hazard anaonekana yuko vizuri. Costa anaonekana yupo vizuri pia. Wote wakiendelea kuwa fiti watakuwa na nafasi nzuri ya ubingwa,” aliongeza Neville.

Mechi inayofuata Jumapili ijayo Chelsea watakuwa nyumbani wakiwakaribisha West Brom na Jumatano watakuwa ugenini na Sunderland ambayo inaonekana kufufuka chini ya Kocha David Moyes kwa sasa.