#WC2018: Ule utamu umerudi!

Muktasari:

Ukimtaka Cristiano Ronaldo, Eden Hazard, Mohamed Salah, Kevin De Bruyne na hata Mesut Ozil na Paul Pogba nao utawakuta Russia. Kutamu huko, si mchezo. Wakali hao watakuwa na vikosi vya timu ya taifa, ambavyo vitakuwa 32 tofauti, vitakavyowania taji moja tu lenye heshima kubwa duniani, Kombe la Dunia.

ULE utamu umerudi. Utamu wa kuwaona mastaa wote wa soka wanaotamba sehemu mbalimbali duniani wakikutana kuonyesha ubabe kwenye nchi moja, kwenye Kombe la Dunia na safari hii, vita itapigwa huko Russia.Unataka Lionel Messi, utamkuta Russia.

Ukimtaka Cristiano Ronaldo, Eden Hazard, Mohamed Salah, Kevin De Bruyne na hata Mesut Ozil na Paul Pogba nao utawakuta Russia. Kutamu huko, si mchezo. Wakali hao watakuwa na vikosi vya timu ya taifa, ambavyo vitakuwa 32 tofauti, vitakavyowania taji moja tu lenye heshima kubwa duniani, Kombe la Dunia.

Timu zenyewe ni Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia kutoka Afrika, wakati timu za mabara mengine ni Australia, Iran, Japan, Korea Kusini, Saudi Arabia, Ubelgiji, Croatia, Denmark, England, Ufaransa, Ujerumani, Iceland, Poland, Ureno, Russia, Serbia, Hispania, Sweden, Uswisi, Costa Rica, Mexico, Panama, Argentina, Brazil, Colombia, Peru na Uruguay ya Luis Suarez na Edinson Cavani.

Ujerumani ndiyo bingwa mtetezi. Watabeba tena? Tusubiri kuona kitakachotokea. Bingwa anavuna Dola 38 milioni ( Sh 85.3 bilioni). Timu itakayotolewa katika makundi itapewa Dola 8 milioni (Sh17.9 bilioni), itakayotolewa hatua ya 16 bora itapata Dola 12 milioni (Sh26.9 bilioni) na itakayotolewa katika robo fainali itapata Dola 16 milioni (Sh35.9 bilioni).

Timu itakayoshika namba nne itapata Dola 22 milioni (Sh 49.3bilioni), nafasi ya tatu Dola 24 milioni (Sh53.8 bilioni), mshindi wa pili Dola 28 milioni (Sh 62,8 bilioni). Sambamba na hilo kuna tuzo pia za mchezaji mmoja mmoja kulingana na ubora.