Mabondia wa Taifa wanacheekaa

Monday March 5 2018

 

ULE msoto wa kushindia chai na chapati sasa umegeuka historia kwenye kikosi cha ndondi cha taifa kinachojiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola.

Mabondia hao sasa wanacheka tu kwenye kambi yao iliyoanza juzi Jumamosi kule Kibaha mkoani Pwani.

Iko hivi. Mabondia hao wa timu ya Taifa wanaojiandaa na michezo ya Madola itakayoanza Aprili 4 mpaka 15 wameonja tena ladha ya kuingia kambini baada ya kuikosa kwa kwa miaka kadhaa.

Baada ya kambi hiyo kuanza cha kwanza walichotamka ni kwamba: “Kambi ina raha jamani, sasa hivi ni tizi kwa kwenda mbele, hadi tulete medali.”

Kama haitoshi, nahodha msaidizi akasisitiza kuwa pamoja na kwamba wamechelewa kuanza kambi, hiyo siyo ishu watakachokifanya ni kuhakikisha wanajitoa ili mradi tu kurejesha heshima ya mchezo huo kimataifa.

Yote tisa, kwenye kambi hiyo sasa labda mabondia washindwe wenyewe, kuna gym ya mazoezi yenye kila aina ya vifaa, lakini hata wakitaka ulingo kwa ajili ya ‘sparing’ upo, msosi sio wa ‘kuunga unga’ kama ilivyokuwa awali.

Menyu yao asubuhi ni chai ya maziwa na maini, chapati, tambi, matunda wakati mwingine mayai, mchana sasa wanakula ugali, wali, ndizi, samaki, kuku, matunda, mboga za majani na usiku menyu ni hiyo hiyo ingawa inabadilika kidogo na kuna chai ya saa 10 jioni.

Habari mbaya kwao ni kwamba, nchini Australia kwenye michezo hiyo hawataongozana na makocha wao wanaowafundisha mazoezi na badala yake wataambatana na kocha kutoka Kenya, huku habari za chini chini zikibainisha kwamba makocha hao wazawa hawana vigezo.