Kili Marathoni usipime, ni zaidi ya mbio

Monday March 5 2018

 

By IMANI MAKONGORO

ACHANA na matokeo ya jana ya mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathoni (Kili marathoni) zilizofanyika jana kwenye viwanja vya Chuo kikuu cha Ushirika, Moshi, kubwa kuliko ni jinsi mbio hizo ‘zilivyouteka’ mkoa wa Kilimanjaro.

Unaambiwa ilikuwa ni zaidi ya mbio, zilitikisa mji wote wa Moshi na maeneo jirani, lakini pia kufungua fursa ya mbalimbali za biashara.

Wingi wa wanariadha kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi ulikuwa gumzo huku waandaaji wakisisitiza kuwa zimefanyika kwa mafanikio.

“Tulikuwa na Wanariadha zaidi ya 10,000 kutoka nchi zaidi ya 40 walioshiriki mbio hizo,” alisema Mkurugenzi wa kampuni ya Executive Solutions inayoandaa mbio hizo, Aggrey Marealle.

Shamrashamra ya mbio hizo zilianzia njia panda ya Himo hadi Moshi Mjini ambako maeneo mengi ya mji huo yalipambwa na bendera zilizotangaza uwepo wake.

Sio Bodaboda, wafanyabiashara wa hoteli, chakula na huduma nyingine za kijamii wa mjini Moshi na maeneo jirani walitumia fursa hiyo ‘kupiga’ mkwanja huku pia nchi ikijitangaza kiutalii.

Ndani ya uwanja, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamadunia na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alikuwa kivutio baada ya kuanzisha mbio hizo kwa kukimbia zile za Grand Malt kilomita tano sanjari na katibu mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na wadau mbalimbali wa riadha nchini.

Kivumbi kilikuwa kwenye mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon (kilomita 42) na zile za Tigo nusu marathoni (kilomita 21), ambazo pia Shirikisho la riadha Tanzania (RT) limepanga kuwachukua nyota wa Tanzania waliofanya vizuri kuongeza nguvu kwenye timu ya taifa itakayochuana kwenye mashindano ya dunia ya nusu marathoni ya Machi 22 nchini Hispania.

“Mafanikio ya mbio hizo yametokana na malengo ambayo tuliyaweka tangu zinaanzishwa kwa kushirikiana na wadhamini wetu,” alisema Marealle na kuendelea.

“Kama waandaaji tunafarijika kuona muitikio mkubwa wa washiriki ambao wameendelea kuifanya mbio kuwa kubwa na za kuvutia kimataifa hivyo kasi hii itaendelea zaidi na zaidi kwenye mbio zijazo,” alisema.

Waziri Mwakyembe aliwapongeza waandaaji wa mbio hizo sanjari na wadhamini wao kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, Tigo, First National Bank, Kilimanjaro Water, Diamond Motors Ltd, Kibo Palace, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Simba Cement, KNAUF Gypsum na AAR kwa mafanikio ya mbio hiyo.

“Naiona riadha ya Tanzania katika sura ya tofauti, naamini kwa hamasa iliyoonekana kwenye mbio za Kili marathoni ni kiashiria tosha cha mafanikio, hongereni sana waandaaji na wadhamini,” alisema Mwakyembe.